
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi leo mbele ya waandishi wa habari kocha
mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark ambaye
amechukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anainoa Taifa Stars.
Michelsen ambaye amepewa mkataba wa
mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema
falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote
wa mchezo.
Kabla ya kuja Tanzania, Michelsen
alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A
ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa
vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja ya mafanikio yake ni kuipa
ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya
miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.