Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
KITENGO cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kinachunguza Sh303.7
bilioni ambazo zinadaiwa kukutwa kwenye akaunti sita za Watanzania,
wakiwamo wanasiasa, katika benki mbalimbali nchini Uswisi.
Chanzo
cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya Interpol kilichonukuliwa na
gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, kimesema baadhi ya wanasiasa
nchini na watu wengine ndiyo wanahusika na ufisadi huo kwa kuwa na
akaunti zenye fedha nyingi nchini Uswisi.
Fedha hizo zimeelezwa
ziliingizwa katika akaunti hizo na kampuni za uchimbaji mafuta na
kampuni za uchimbaji madini, ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti, zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa.
Kiasi
hicho cha fedha kilichofichwa Uswisi, kinatosha kuendesha Bajeti ya
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitano, au kusaidia Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuendesha shughuli zake kwa miaka
miwili.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti
hizo zifunguliwe wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi
moja.
"Wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na
kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa
nchini," kilidokeza chanzo hicho.
Mabilioni hayo yamebainika
kufichwa wakati takwimu zilizotolewa na Umoja wa Taasisi za Kupambana na
Rushwa barani Afrika ikiwamo Tanzania, zikionyesha kwamba Sh22
trilioni, zimekuwa zikitoroshwa nchini humo na kufichwa katika nchi za
kigeni, ikiwamo Uswisi.
Fedha hizo zimebainishwa na ripoti ya
Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikibainisha
nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zake
zilizohifadhiwa huko.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) hivi sasa inafuatilia suala hilo kwa mamlaka za Uswisi, ili
kujua fedha hizo ziliko na nani anazimiliki.
Mbali ya Tanzania,
nchi nyingine ambazo zina fedha nyingi katika benki za Uswisi ni Kenya
(dola 857 milioni), Uganda (dola 159 milioni), Rwanda (dola 29.7
milioni) na Burundi dola 16.7 milioni.
Jumla ya fedha zilizoko katika
benki za Uswisi kutoka nchi hizo nyingine za Afrika ni Faranga 1.53
trilioni za nchi hiyo na ripoti hiyo imeelezwa kuwa kuna msukumo wa
kimataifa wa kuitaka nchi hiyo izitake benki zake, kubadilishana taarifa
za wateja na serikali za kigeni.
Ripoti hiyo imekuja wakati pia
Uswisi ikiwa na rekodi ya kuhifadhi mabilioni ya dola kutoka nchi za
kigeni ikiwamo Afrika, kwani iliwahi pia kuhifadhi dola zaidi ya bilioni
1.5 za aliyekuwa Kiongozi wa Kijeshi wa Nigeria, Jenerali Sani Abacha
na dikteta Mobutu Seseseko wa iliyokuwa Zaire.
Gavana azungumza
Akizungumzia
ripoti hiyo, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu (pichani)
alisema uamuzi huo wa Uswisi wa kuanza kufungua milango utaiwezesha BoT
kuwa na rekodi ya kiasi halali cha fedha zilizopo katika nchi hiyo.
Profesa
Ndulu alifafanua kwamba katika siku za nyuma, Uswisi haikuwa imefungua
milango kwa kutaja kiasi cha fedha za wateja wake walioweka fedha katika
benki zake, hivyo ilikuwa vigumu kwa mamlaka za ndani kuweza kufanya
uchunguzi.
"Ndiyo kwanza wameanza kufungua milango, sisi siku
zote tulikuwa hatuwezi kujua nini kinaendelea. Lakini, angalau sasa
tutaweza kujua na kuwa na rekodi baada ya uamuzi huo wa kufichua kiasi
cha fedha kilichomo katika benki zake," alifafanua gavana.
Kiutaratibu, BoT inapaswa kuwa na rekodi ya fedha halali za Watanzania zilizopo nje ya nchi.
Kauli ya Takukuru
Mkurugenzi
Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikaririwa na The Citizen hivi
karibuni alisema kuwa ofisi yake ina taarifa kuhusu suala hilo na kwamba
wanaanza mawasiliano na Serikali ya Uswisi kujua ukweli wake.
Dk
Hoseah alisema taasisi hiyo inataka kujua jinsi gani fedha hizo
ziliwekwa kwenye benki za Uswisi, watu waliohusika na namna uhamishaji
wa fedha hizo ulivyofanyika.
"Tutakapogundua fedha hizo zimetoka
wapi, tutafuata taratibu zinazohusika kuhakikisha zinarudi nchini,"
alisema Dk Hoseah na kuongeza: "Tutatumia sheria zilizopo katika nchi
hizi."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Kamishna Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akieleza
kuwa yuko likizo, hivyo aulizwe msemaji wa Jeshi la Polisi.
Msemaji
wa jeshi hilo, Advera Senso alisema hawajapata ripoti hiyo na kwamba
atawaomba watu wa uchunguzi kumpatia, ili aweze kutoa taarifa.
SOURCE: MWANANCHI
June 26, 2012
VIGOGO WALIOFICHA BILLION 300 USWIZI SASA HADHARANI
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget