Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiitikia dua
baada ya kushiriki futari iliyoandaliwa na Masjid Iman iliyoko Mbweni
Zanzibar.Katikati ni Sheikh Habib Ali Kombo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akifurahi pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso
Lenhardt, aliyefika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kubadilishana
mawazo. Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
---
Balozi
wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt ameahidi nchi yake
itaunga mkono juhudi za Zanzibar kuwa na mipango madhubuti ya uokoaji
wakati yanapotokea majanga, ili kunusuru maisha ya watu pale inapotokea
hali kama hiyo.
Amesema msaada wa Marekani utaelekezwa zaidi kuiwezesha Zanzibar
kuwa na mfumo wa kisasa wa mawasiliano utakaosaidia kujua eneo la
tukio na kumudu kufika kwa haraka, kwa nia ya kuokoa maisha ya watu
wengi zaidi iwezekanavyo.
Balozi Alfonso amesema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad huko
nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar kuzungumzia tukio
la kuzama kwa meli ya MV. Skagit, pamoja na mambo mengine mbali mbali.
“Msaada huu wa kuepusha maafa wakati yanapotokea majanga, utakuwa ni
kwa Tanzania nzima, lakini tutahakikisha Zanzibar inanufaika nao na
inajijengea uwezo wa kuokoa maisha ya watu wake, wakati wa maafa kama
haya ya kuzama kwa meli na mengineyo”, aliahidi Balozi Lenhardt.
Hata hivyo, Balozi huyo wa Marekani alisifu mshikamano wa
wananchi wa Zanzibar pamoja na serikali yao, wakati wa maafa ya kuzama
kwa MV. Skagit mwezi uliopita, hali ambayo ilisaidia kuokolewa baadhi
ya watu waliokuwemo kwenye meli hiyo.
Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad amekaribia azma hiyo ya Marekani kuisaidia Zanzibar katika
kukabiliana na majanga mara tu yanapotokea. Katika hatua nyengine
Balozi Lenhardt ameisifu Zanzibar kwa hatua kubwa iliyoweza kufikia
kudhibiti ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo vya watu
wengi wakiwemo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Balozi huyo amesema Zanzibar imejijengea heshima na hivi sasa
imekuwa mfano Duniani na wataalamu kutoka sehemu mbali mbali wanakuja
Zanzibar kujifunza mbinu za kutokomeza ugonjwa huo. Akizungumiza
mafanikio hayo, Maalim Seif alisema suala la elimu kwa wananchi juu ya
kutokomeza ugonjwa huo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na uelewa wa
hali ya juu kujilinda wasipate maradhi hayo.
Maalim Seif alisema baada ya wananchi walio wengi kuelewa mbinu
za kujikinga na Malaria imekuwa rahisi kuweza kuzitumia njia
wanazoshauriwa na wataalamu.
Alizitaja baadhi ya mbinu hizo kuwa ni matumizi ya vyandarua,
kupuliziwa dawa kwenye nyumba zao, kuweka mazingira yao katika hali ya
usafi pamoja na kufika kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na kutibiwa
mara wanapoona dalili za kuwa na maradhi hayo.
Balozi huyo wa Marekani pia amemhakikishia Makamu wa Kwanza wa
Rais kuwa nchi hiyo itaendelea kufanikisha miradi mbali mbali
inayofadhiliwa na Marekani hapa Zanzibar.
Miongoni mwa miradi hiyo ni utandikaji wa laini kuu ya umeme
kutoka Dar es Salaam hadi Fumba kupitia chini ya bahari na ujenzi wa
barabara tafauti, ambayo yote ipo katika hatua nzuri za utekelezaji.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais jana alijumuika katika
futari iliyoandaliwa na masjid Iman iliyoko mbweni, nje kidogo ya mji
wa Zanzibar.
Futari hiyo iliwajumuisha wananchi mbali mbali wanaosali katika
msikiti huo pamoja na viongozi kadhaa wa dini na siasa wakiwemo Sheikh
Habib Ali Kombo na Makamu Mwenyekiti wa CUF Machano Khamis Ali.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!