Mabingwa
watetezi Uhispania wamefuzu kuingia fainali ya Euro 2012, baada ya
kuishinda Ureno magoli 4-2, kupitia mikwaju ya penalti, baada ya muda wa
kawaida wa dakika 90 na dakika 30 za ziaida kumalizika kwa timu hizo
mbili kushindwa kufungana.
Bao
la mwisho la mikwaju ya penalti kwa Uhispania lilitiwa wavuni na Cesc
Fabregas, na kuwapa wenzake matumaini ya kutetea ubingwa wao kikamilifu,
watakapocheza aidha na Ujerumani au Italia katika fainali ya Jumapili.
Fabregas,
ambaye ni kiungo cha kati wa timu ya Barcelona, alipiga mkwaju ambao
baada ya kugonga mwamba upande wa kushoto, ulitambaa wavuni, na ikawa ni
tiketi ya Uhispania kufanya mipango ya kusafiri hadi Kiev, Ukraine, kwa
fainali.
Mchezaji
wa Ureno, Bruno Alves, alielekea kuwa na wasiwasi, na kushindwa kufunga
mkwaju wake, baada ya mpira kugonga mwamba, na Ronaldo, akiwa amepangwa
na timu yake katika nafasi ya tano kwa wapigaji penalti, hakupata hata
nafasi ya kutimiza wajibu huo.
Wengine
waliokosa kufunga kupitia mikwaju ya penalti ni mchezaji wa Ureno, Joao
Moutinho, wakati kipa wa Uhispania, Casillas, alipoweza kuokoa kwa
kuruka upande wa kkulia.
Awali
mchezaji wa Uhsipania Xabi Alonso naye alikosa kutumbukiza wavuni
mkwaju wa penalti, licha ya kwamba ulikuwa ni mkwaju wa kasi na
uliopigwa kwa nguvu, lakini kipa Rui Patricio akauzuia.