Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeanza ziara ya siku
14 katika balozi za Tanzania kwenye nchi za Marekani, Ulaya na Asia
kukagua namna zinavyotekeleza mambo ya sera na uchumi.
Ziara ya
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
ilitangazwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), jijini Dar ers Salaam wakati wajumbe 20 wa Kamati hiyo na
makatibu sita wanaondoka nchini.
Hata hivyo, wakati Kamati hiyo
ikienda kutembelea balozi hizo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe mwenye dhamana na balozi hizo, alisema ziara
hiyo haikuja wakati sahihi, kwa kuwa Mkutano wa Bunge la Bajeti
unaendelea.
Lakini, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
ziara hiyo, Lowassa alisema ziara hiyo imekuja wakati sahihi kwa kuwa
hiyo pia ni kazi ya Bunge.
Katika ziara hiyo, Kamati hiyo
imegawanyika katika makundi sita yatakayotembelea balozi 14 katika nchi
14. Wabunge hao ni yeye Lowassa, Vita Kawawa, Khalifa Suleiman
Khalifa, Rachel Mashishanga na Beatrice Shelukindo ambao watatembelea
balozi za Canada, Washington na New York, Marekani na London, Uingereza.
Wengine ni Mohamed Ibrahim Sanya, Mchungaji Israel Natse ambao watatembelea New Delhi, India na Kuala Lumpur, Malaysia.
Kundi
jingine lina Mussa Zungu, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Betty
Machangu na Mussa Hassan Mussa linaotembelea balozi za Japan na China.
Kundi
la nne litakalotembelea Ujerumani na Sweden, linawahusisha Anna
Abdallah, John Shibuda na Augustino Massele, huku wabunge wengine
akiwamo Mohamed Seif Khatib, Hilda Ngoye na Anastazia Wambura
watatembelea balozi za Brussels, Ubeligiji na Geneva, Uswisi.
Kundi
la mwisho linalotembelea Paris Ufaransa na Rome Italia, linawahusisha
wabunge John Chiligati, Engen Mwaiposa na Masoud Abdallah Salim.
Kauli ya Membe
Ziara hiyo imeonyesha kumshangaza Waziri Membe akisema kuwa hajui wanakwenda kufanya nini huko.
Akizungumza
na gazeti dada la The Citizen jana katika uwanja huo, Waziri Membe
aliyekuwapo katika uwanja huo, alisema ziara hiyo haikuja wakati sahihi.
“Shughuli za Kamati huko nje huwa ni kujifunza kutoka kwa
wenzao kwenye mataifa tofauti, na ziara hii hilo halikufanyika….lakini
nimesikia wanakwenda kutembelea balozi zetu huko nje na sio zilizoko
katika bara la Afrika,” alisema Waziri Membe.
Aliongeza kuwa,
“Hapo inabidi sote tujiulize kama lengo ni kuangalia utendaji wa balozi
zetu mbona sasa zinakuwa za Ulaya na Asia peke yake?"
Waziri
Membe alifafanua kuwa kwenda kutembelea balozi si tatizo, lakini katika
kipindi hiki ambacho Bunge la Bajeti linaendelea mjini Dodoma, kwa
busara ya kawaida, mbunge anatakiwa kuwa bungeni akifuatilia Bajeti.
Alisema
kulingana na ratiba ya Bunge, ziara kama hiyo ilitakiwa kufanyika
wakati wa vikao vya Kamati za Bunge, lakini si sasa ambapo Bunge
linakutana.
Licha ya kukanusha mara kwa mara, Waziri Membe na
Lowassa wamekuwa wakitajwa kuwania Urais kupitia CCM siku za usoni,
jambo ambalo limekuwa likiwataja wabunge hao kama mahasimu wa kisiasa.
Kilichotokea kwenye kamati
Tayari
Kamati hiyo imewahi kuripotiwa kuingia katika mvutano Membe, ambapo
Juni 6, mwaka huu ilimbana ikisema alichelewa kugawa vitabu vya bajeti
yake kwa wajumbe wa Kamati.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo
aliliambia gazeti hili kwamba wajumbe waligomea Bajeti hiyo kutokana na
kuchukizwa na kitendo hicho na kutokuonyesha madeni ya wizara yakiwamo
makato ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Ofisa
Habari na Mawasiliano wa Wizara hiyo, Assah Mwambene alipinga taarifa
hizo, lakini akafafanua kilichotokea kuwa hoja ya vitabu kuchelewa
iliibuka, na tayaru waziri aliwaeleza wajumbe kuwa hilo ni suala ambalo
lilitokana na kamati husika.
Alisema vitabu hivyo
viliwasilishwa mwisho wa wiki, lakini kwa kuwa labda haikuwa siku za
kazi, ndiyo maana havikuwafikia mapema wajumbe.