Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
RAIA 45 wa Ethiopia wamekufa na wengine 72 wako taabani baada ya kukosa hewa katika lori walilokuwa wakisafiria kwenda Malawi.
Maiti
za watu hao na wenzao ambao wako katika hali mbaya, waligundulika jana
asubuhi katika msitu wa Chitego wilayani Kongwa, Dodoma.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alithibitisha jana
tukio hilo baada ya kufika katika eneo hilo na msafara wa polisi,
akiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen.
Silima
aliitaja idadi ya watu waliokufa kuwa ni 45 na kuwa wengi wao walikuwa
katika umri mkubwa. Vijana walinusurika, lakini nao walionekana
kudhoofu, alisema.
“Ni kweli niko katika eneo la tukio,
inasikikitisha watu hawa wamekufa vibaya. Inaonyesha kuwa walikufa kwa
kukosa hewa wakiwa ndani ya lori, lakini bado tunafanya uchunguzi zaidi
ikiwa ni pamoja na kusaka roli hilo ambalo lilitokomea kusikojulikana,’’
alisema Silima.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa uchunguzi wa
awali ulionyesha kuwa watu hao walikuwa wakifa mmoja baada ya mwingine
na dereva alipogundua hilo aliona hakuna namna zaidi ya kuwatupa porini.
Alisema
kitendo cha kusafirisha watu hao kimekuwa ni mchezo wa kawaida kwani
Watanzania ndio wanaosaidia kuwasafirisha kutoka Nairobi kupitia Arusha
na mara nyingi hupita usiku katika njia za panya.
Kwa mujibu wa
Silima, miili ya watu hao ilichukuliwa jana na kupelekwa kwa ajili ya
uchunguzi huku wakitafuta mawasiliano na Ubalozi wa Ethiopia ili kuona
namna watakavyofanya.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya
alithibitisha kupokea maiti hiyo na wengine walio hai kupewa msaada wa
kimatibabu.
Dk Mpuya alisema katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
alitegemea kupokea maiti 25 na wagonjwa wawili waliokuwa katika hali
mbaya, huku maiti 20 zilitarajiwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro kwa uchunguzi zaidi.
Mganga huyo alisema watu wengine
ambao walionekana kuwa na hali nzuri kidogo wangepita hospitalini hapo
na kupewa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa kwenye vyombo vya sheria
kwa mahojiano zaidi.
Chanzo: Mwananchi