PICHA NA MAKTABA |
|
MTWARA MIRINDIMO ya Mabomu ya machozi imesikika usiku kucha katika kijiji cha Mahuta wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara baada ya wananchi wenye hasira kali kuchoma moto Pikipiki ya Polisi inayodaiwa kugonga watoto wawili kijijini hapo. Habari kutoka kijijini hapo zinadai kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia (leo) jana ambapo polisi wanadaiwa kutumia mabomu ya machozi kutuliza jazba za wananchi zilizochagizwa na polisi kugonga watoto hao na kumjeruhi mmoja kwa risasi, juzi mchana walipojaribu kumkimbiza mwendesha Pikipiki kwa lengo la kumkamata. Shuhuda wa tukio hilo wameliambia gazeti hilo kwamba polisi wawili wakiwa wamepakizana kwanye Pikipiki huku mmoja akiwa amebeba Bunduki walikuwa wakimkimbiza mwendesha pikiki kwa lengo la kumkamata na ndipo walipowagonga watoto wawili waliokuwa wamepakizana kwenye baiskeli. “Baada ya kuanguka polisi wakiamka haraka kwa lengo la kukimbia, lakini hawakufanikiwa, tayari wananchi walikuwa wamewazingira…aliyebeba silaha baada ya kuona watu wanaongezeka alifyatua risasi, na kumjeruhi katika paja la kushoto ,Bwatam Nambenge (22)” alieleza Mohamedi Chivalavala shuhuda wa tukio Aliongeza kuwa “Polisi walikimbilia kituo cha polisi na kuiacha Pikipiki, wananchi kwa hasira waliamua kuichoma moto, baadae wananchi walizingira kituo cha polisi wakiwa wamebeba mawe wakitaka kuwaadhibu polisi waliosababisha ajali hiyo” Shuhuda huyo aliwataja watoto waliogongwa kwa Pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na polisi hao kuwa ni Bibie Hassan (15) na Faima Mkumba (9) wote wakazi wa kijiji cha Mahuta. Kwa mujibu wa mganga wa Kituo cha Afya Mahuta, Edina Chibwana watoto hao wanaendela na matibabu vizuri pamoja na majeruhi wa risasi. Habari zaidi zinadai kuwa muda mfupi baadaye polisi kutoka wilaya jirani ya Newala na Mtwara waliwasili kijijini hapo kuwasaidia wenzao ambapo walifyatua mabomu ya machozi hewani usiku kucha na hivyo kusababisha hofu kwa wananchi na wengine kuyakimbia makazi yao . “Hatukulala kabisa, polisi wamekesha wakifyatua mabomu ya machozi hewani, hakuna amani kabisa, hali ni tete…watoto na vikongwe wamelala porini” alieleza Chivalavala Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Ponsiano Nyami ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa atatoa taarifa baada ya kurudi kwenye eneo la tukio. “Kuna taarifa zenye mkanganyiko, kwa mfano wapo wanaosema polisi wamempiga risasi raia kwa makusudi, wengine wanasema alijeruhiwa kwa bahati mbaya, zipo taarifa kituo kimechomwa moto, wengine wanasema kipo salama… Wapo wanaosema watoto wapo mahututi wengine wanaendelea vizuri, wapo wanaosema askari mmoja yupo hoi wengine anaendelea vizuri sasa ni lazima nifike huko ili nitoe taarifa yenye usahihi” alisema Nyami Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuiita kwa mda mrefu bila majibu. |
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!