Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame Yanga wamepangwa kundi mchekea,
huku mahasimu wao Simba wakitupwa kundi la kifo katika mashindano hayo
yatakayoanza kupigwa Julai 14 jijini Dar es Salaam.
Mashindano
hayo ambayo kwa mwaka wa tatu mfululizo yanafanyika katika ardhi ya
Tanzania yatashirikisha timu 11 ikiwamo APR (Rwanda),Wau Salaam (Sudan
Kusini), Atletico (Burundi), Simba, Yanga, Azam (Tanzania),
Tusker(Kenya), Ports (Eritrea), URA (Uganda) na Vital Club ya Congo DRC.
Ikitokea
kundi C, Yanga itafungua pazia la mashindano hayo kwa kuwakabili
mabingwa wa Burundi timu ya Atletico katika pambano litakalopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 8 mchana kabla ya baadaye jioni
kushuhudiwa mechi nyingine za kundi hilo kati ya Wau Salaam ya Sudan
Kusini na APR ya Rwanda.
Kwa upande mwingine, Simba iliyoswekwa
kundi A itasubiri hadi Julai 16 pale itakapokwaana na mabingwa wa Uganda
timu ya URA katika pambao litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Vigogo wengine wanaokamilisha kundi C mbali ya Simba na URA ni Vital Club ya Burundi na mabingwa wa Djibout,Ports.
Kwa
mujibu wa Ratiba ya Mashindano iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), washindi wa
pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Azam FC wamepangwa kundi B pamoja na
timu za Mafunzo na Tusker ya Kenya.
Azam FC ambayo itashiriki
mashindano hayo kwa mara ya kwanza, itaanza kampeni yake Julai 15 kwa
kukwaruzana na Mafunzo katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa
Chamazi Complex nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Timu nane
zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A
na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati kundi B
litatoa timu mbili.
Katika hatua nyingine, Musonye alisema timu
za El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman
ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu kutokana na
sababu tofauti.
Akifafanua zaidi, Musonye alisema Coffee
imeshindwa kushiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14, wakati
El Merreikh inakabiliwa na mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika
(Caf).
Alisema Cecafa imeiondoa Red Sea kutokana historia ya
wachezaji wa timu hiyo kutokomea kusikojulikana baada ya kuondolewa
mashindanoni na kudai kwamba ukosefu wa amani nchini Somalia kama sababu
za Elman kutoshiriki.
Bingwa wa mashindano hayo atapata dola
30,000, wakati mshindi wa pili atapata Dola 20,000 huku yule wa tatu
ataondoka na dola 10,000.