Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
TUKIO la kujeruhiwa vibaya Dk Stephen Ulimboka, jana kulilichochea
hasira ya madaktari ambapo kundi la madaktari liliingia wodi hadi wodi
katika hospitali ya rufaa ya KCMC na kuwatoa madaktari kazini.
Taarifa
zilizopatikana hospitalini hapo zilisema, madaktari hao waliwatoa kwa
nguvu wenzao waliokuwa wakiendelea kutoa huduma katika hospitali hiyo
wakiwamo madaktari raia wa kigeni.“Ni balaa maana madaktari wameingia
wodi moja hadi nyingine hadi wodi ya wazazi na kutushurutisha tusitishe
kutoa huduma kama njia ya kupinga kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka”,
alidai mmoja wao.Madaktari hao walikuwa wakitembea na Laptop
zikiwa na picha za Dk Ulimboka, akivuja damu huku wengine wakiwa na
picha zilizochapishwa kwenye karatasi wakionyesha kila mtu wanayekutana
naye.
Madaktari hao walikusanyika katika mgahawa uliopo jirani na
chumba cha kuhifadhia huku wakipaza sauti wakitaka tukio la Dk Ulimboka
liweke historia nchini katika kupigania haki za madaktari.
Huku
wakikataa kupigwa picha wala kunukuliwa majina yao, madaktari hao
wamesema watasitisha kutoa huduma zote zikiwamo za dharura kama Serikali
haitatoa kauli ya kuridhisha juu ya tukio hilo.
“Pinda
(Mizengo-Waziri Mkuu) si amesema liwalo na liwe basi na sisi tunasema
haturudi kazini kwa sababu usalama wetu ni mdogo na sisi tunasema liwalo
na liwe”walisikika madaktari hao wakisema.
Hata hivyo madaktari
katika hospitali za serikali na vituo vya Afya katika wilaya za Same,
Mwanga,Rombo, Hai na Moshi waliendelea kutoa huduma kama kawaida huku
wakisita kutoa maoni yao juu ya tukio hilo.
Waandishi
walipotembelea wodi mbalimbali na kuzungumza na wagonjwa, walisema wengi
wao wameruhusiwa japo hawajapona na vitanda vingi hospitalini hapo
vimebaki vitupu.
Mgomo katika hospitali hiyo ulianza Jumatatu
wiki hii, ukihusisha madaktari walioko kwenye majaribio wapatao 80
lakini tukio la Dk Ulimboka limechochea hasira hadi za madaktari bingwa.
“Tunasubiri
tamko la Serikali lakini isipofanya hivyo hata sisi hatuwezi kuingia
kazini maana hili ni tukio la kinyama sana…hatuaamini kama ni Tanzania”,
alisema mmoja wa madaktari bingwa.
Baadhi ya wagonjwa waliokuwa
wamepewa rufaa kutoka hospitali mbalimbali kwenda KCMC, jana walijikuta
wakirudishwa walikotoka kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea
hospitalini hapo.
Mbali na kutopokelewa kwa wagonjwa wapya
wanaohitaji kulazwa, lakini kliniki zote za wagonjwa wa kisukari, ukimwi
na wale waliofanyiwa operesheni zimefungwa rasmi kutoa huduma kwa
wagonjwa.
CHANZO: MWANANCHI