(Picha na maktaba)
KITENDO cha kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk Stephen Ulimboka, kumeibua hisia kali kwa madaktari waliopo
katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, huku wakisema kuwa Serikali haiwezi
kukwepa kuhusiana na kitendo hicho.Wakizungumza na Mwananchi, madaktari waliogoma hospitalini hapo huku wakikataa kabisa kuandikwa majina yao walisema, watanzania wanatakiwa kutambua wazi kwamba Serikali imetangaza vita na madaktari hao na kwamba wameitaka Serikali kutolea ufafanuzi yakinifu kuhusiana na kupigwa kwa kiongozi huo.
Walisema kitendo cha kutekwa kwa Dk Ulimboka, kamwe hawapo tayari kurudi kazini licha ya kuwa baadhi yao walikuwa tayari kurejea kazini lakini kutokana na hilo hawawezi kumsaliti Ulimboka kwa kitendo alichofanyiwa, na kudai kuwa ndio kwanza mgomo huo umeanza rasmi sasa uliopita haukuwa mgomo.
“Kamwe sisi hatupo tayari kurudi kazini tena, kwanza ndio mgomo umeanza rasmi na kutokana na hali hii watanzania watambue wazi kwamba serikali imechoka, tumetoka vijijini tutarudi kulima, lakini hatutamsaliti Ulimboka” alisema mmoja wa madaktari hao huku akitokwa machozi.
Daktari huyo ambaye yupo katika mafunzo ya vitendo alisema kuwa kumpoteza Dk Ulimboka siyo mwisho wa kudai haki kwa kuwa ulimboka ni kiongozi tu na suala la kudai maslahi yao yapo mikononi mwao hivyo wataendelea na harakati zao hadi kitakapo eleweka.
“Kumwagika kwa damu ya Ulimboka kumetengeneza akina Ulimboka wengi na damu yake italipwa na sisi kwa kutomsaliti kwa namna yoyote ile na hiyo damu ya mpigaji mwenzetu ndio kwanza imefumbua makucha yetu kuanzia sasa” alisema daktari huyo.
Hata hivyo, Daktari bingwa ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe alisema, kitendo cha kutekwa kwa Dk Ulimboka hata wao ambao hawakuwapo katika mgomo huo sasa, wanaingia kwenye mgomo huo rasmi kwa kile alichodai kuwa ulimboka ni daktari kama wao.