Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimelaani kukamatwa na
kushambuliwa kwa viongozi wa madaktari ikiwamo Dk Ulimboka Steven
ikieleza kuwa hatua hiyo haiwezi kuwa suluhu bali itachochea zaidi
mgogoro wa madaktari na Serikali. Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika inaeleza pia kwamba udhaifu
wa Serikali kuharakisha kwenda mahakamani kabla ya Bunge kupewa fursa
ya kujadili madai ya madaktari na kuisimamia Serikali umelifikisha taifa
katika hali iliyopo sasa.
"Nalaani uamuzi wa Serikali wa kutumia
vyombo vya dola kukamata na kushambulia viongozi wa madaktari ikiwemo
Dk Ulimboka Steven kwa hauwezi kuwa suluhu bali utachochea zaidi mgogoro
kati ya madaktari na Serikali," ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo ya
Mnyika na kuongeza:
“Nichukue fursa hii kuwaomba madaktari
kufanya kila kinachowezekana kuokoa uhai wa wagonjwa katika kipindi hiki
kigumu.” Mnyika alisema kuwa ameomba wabunge wapewe nakala ya Taarifa
ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu madai ya madaktari na hoja ya
taarifa husika iwekwe katika orodha ya shughuli za Bunge katika mkutano
wa Bunge unaoendelea ili ijadiliwe na kupitisha maazimio, kuwezesha
hatua za muda mfupi, wa kati na muda mrefu kuupatia ufumbuzi mgogoro huo
na kuboresha sekta ya afya nchini.
“Natarajia kwamba Spika
atawezesha kamati kuwasilisha taarifa yake na Bunge kujadili baada ya
Serikali kutoa kauli yake bungeni,”alisema. Mnyika alisema ikiwa
wabunge wataelezwa ukweli na kupewa taarifa kamili wataweza kuisimamia
Serikali na kuwaeleza ukweli madaktari kipi kinawezekana na kipi
hakiwezekani.
Alisema kuwa ingawa Waziri Mkuu Mizengo Pinda
ametoa maelezo bungeni kuwa Serikali itatoa kauli bungeni kuhusu mgomo
huo, Bunge halitaruhusiwa kujadili kauli husika, hivyo kukoseshwa fursa
ya kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi.