Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Sakata la mgomo
uliotangazwa na madaktari katika hospitali zote za serikali nchini huenda
makali yake yakaongezeka na kuleta athari kwa wagojwa, baada ya Jumuiya ya
Madaktari kusema kuwa huduma zote za dharura zitasitishwa kwenye hospitali zote
nchini kuanzia leo.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk. Stephen Ulimboka, alisema jana kwa njia ya simu
kuwa, huduma za dharura zitasitishwa katika hospitali hizo kutokana na serikali
kutoonyesha nia ya kutatua madai yao kama ilivyotoa ahadi na badala yake kinachofanyika
ni propaganda tu.
Dk. Ulimboka alisema wanashangaa kusikia kuwa serikali imeweka zuio mahakamani
kushinikiza madaktari wasigome, hatua ambayo alidai ni propaganda tu
zinazofanywa na serikali kwani madaktari hawajapewa rasmi taarifa hizo.
“Kauli za serikali na zuio
la mahakama tunazichukulia kama ni propaganda tu, kwanza sababu hilo zuio
hatujalipata rasmi zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari, kwa hali hiyo
kesho (leo) wagonjwa watakuwa na wakati mgumu sana, maana tumekusudia kusitisha
huduma zote za dharura katika hospitali zote nchini, ” alisema.
Alisema ufumbuzi wa mgogoro
wa madaktari na serikali unashindwa kupatikana haraka kwa sababu viongozi wakuu
wa serikali wanaelezwa mambo ya uongo na watu wa chini jambo linalopelekea
kutokuwa na habari sahihi za utekelezaji wa madai yao.
Alisema kutokana na
serikali kupuuza madai yao italazimika kuwajibika kikatiba katika suala la
kuwahudumia wagonjwa ambao wataendelea kupata tabu kwa kukosa huduma za
matibabu.
HUDUMA za matibabu kwa wagonjwa jana ziliendelea kuzorota katika
baadhi ya hospitali, hali iliyotajwa kuwa inatokana na mgomo
uliotangazwa na madaktari.Madaktari walitangaza mgomo wa kutotoa
matibabu nchi nzima kuanzia juzi, wakishinikiza Serikali kutekeleza
madai yao likiwamo la kuboreshewa mishahara na mazingira ya kazi.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH),Taasisi ya Mifupa (MOI) na hospitali nyingine za Jiji la Dar es
Salaam, umebaini kuzorota kwa utoaji huduma.
Katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, uchunguzi ulibaini mbali na ulinzi kuimarishwa,
huduma za matibabu kwa wagonjwa zilizorota, na katika baadhi ya wodi
wagonjwa walikuwa hawajatembelewa na madaktari tangu Ijumaa.
Mmoja
wa watu ambao wanauguza mgonjwa wao katika wodi namba 4 katika Jengo la
Mwaisela, Vicky Rehani alisema mgonjwa wao alipelekwa hospitalini
Ijumaa na hadi jana, alikuwa hajapata huduma yoyote akiwa wodini.
"Mapokezi
kweli alionana na daktari akamuandikia dawa na kulazwa katika wodi hii,
lakini cha ajabu hadi sasa hakuna huduma yoyote ambayo ameipata,"
alisema .
Katika wodi zilizopo katika Jengo la Kibasila baadhi ya
wagonjwa walidai kuwa, kuna madaktari ambao wamefika wodini, lakini
hawakufanya mzunguko kama ilivyo kawaida, na hawakuwa na wasaidizi wao
ambao ni wanafunzi wanaokuwa katika mafunzo kwa vitendo.
Daktari
mmoja aliyekutwa katika wodi ya Sewahaji (alikataa kutaja jina lake),
alipoulizwa kuhusiana na kuwapo kwa mgomo alikataa kusema lolote kwa
madai kuwa si Msemaji wa MNH.
"Siwezi kusema lolote, kwani hata
mimi mwenyewe nimefuata matibabu," alisema daktari huyo na kuongeza kuwa
kama mwandishi anataka kujua kama kuna mgomo au la, basi aende
hospitalini hapo kesho.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi hospitalini
hapo umebaini kupigwa marufuku kwa mikusanyiko ya aina yoyote na hata
bustani inayotumiwa na wagonjwa na jamaa zao ambayo ipo mbele ya Jengo
la Mwaisela, ilikuwa chini ya ulinzi.
"Hapa haruhusiwi mtu yeyote
kukaa, amri hiyo imetoka tangu jana (juzi)," alisema mlinzi aliyekutwa
eneo hilo na kuongeza kwamba hata mikusanyiko ambayo haieleweki imepigwa
marufuku ndani ya eneo la hospitali.
Hali hiyo pia iliwakuta
baadhi ya waandishi wa habari ambao walifika hospitalini hapo na
kujikuta wakizuiwa na walinzi kuingia katika baadhi ya wodi.
Msemaji
wa Hospitali hiyo, Aminieli Eligaesha wakati wote simu yake ilipokuwa
ilikuwa inaita bila kupokelewa, hali ambayo ilijitokeza pia juzi
Jumamosi.
Wakati hali ikiwa hivyo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili na Moi, uchunguzi uliofanywa katika Hospitali za Mwananyamala,
Amana na Temeke ulibaini kuwa huduma ziliendelea kwa kusuasua huku
baadhi ya wahudumu wakisisitiza hatma ya mgomo huo itafahamika leo.
“Ukitaka
kujua sura ya mgomo subiri kesho (leo) itadhihirika kama kweli
madaktari wamegoma au la, lakini kwa leo huduma zinaendelea kwa
kusuasua, bado tunaangalia Serikali itatoa majibu gani,” alisema mmoja
wa madaktari katika Hospitali ya Amana, ambaye hakutaka jina lake
kutajwa.
Aliongeza kuwa jana haikuwa siku ya kugoma, bali ni
kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao na kwamba, kama itaendelea na
msimamo wake huduma zote zikiwamo za dharura zitasitishwa.
Hata
hivyo, huduma katika Hospitali ya Amana jana zilikuwa zikiendelea huku
baadhi ya wagonjwa wakisema kasi ya upatikanaji matibabu ni tofauti na
kipindi ambacho mgomo ulikuwa haujatangazwa.
Katika Hospitali ya
Mwananyamala, hali ya matibabu pia iliendelea kwa kusuasua na
ulipotafutwa uongozi wa hospitali hiyo kuzungumuzia hali hiyo juhudi
hizo hazikuzaa matanda.
Katika Ofisi ya Utawala, mwandishi
alikutana na mmoja wa wafanyakazi ambaye alikataa kutaja jina na kueleza
kuwa Mganga Mkuu alikuwa amekwenda kutembelea wagonjwa wodini.
“Mimi
si msemaji. Hili anaweza kuzungumza Mganga Mkuu, lakini amekwenda
kutembelea wagonjwa wodini na ameniambia akimaliza kazi hiyo anakwenda
kufanya shughuli ya upasuaji, hatakuwa na muda wa kuzungumza nanyi,”
alisema ofisa huyo.
Wakati hali ikiwa hivyo Mwananyamala, katika
Hospitali ya Temeke pia huduma ziliendelea kutolewa huku baadhi ya watu
waliokwenda kuhudumia wagonjwa wao wakibainisha kuwa kasi imepungua.
Katibu
wa Jumuiya ya Madaktari, Edwin Chitage alisisitiza, “Sisi tunaendelea
na mgomo kama kawaida, tutafanya hivyo hadi Serikali itakapotekeleza
madai yetu, na hadi sasa hatujapata taarifa zozote kutoka serikalini,”
alisema Chitage.
KCMC vuguvugu laendelea
Katika
Hospitali ya Rufaa KCMC Moshi, madaktari ambao hawako zamu
wamekubaliana kufanya kikao cha dharura kuhakikisha hakuna daktari
atakayeingia kazini leo.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya
madaktari ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, walisema
wamepanga kufanya kikao cha pamoja ambacho kitaweka mikakati ya jinsi ya
kufanya mgomo mkali leo, tofauti na ilivyokuwa juzi na jana.
“Mgomo
uko palepale kama unavyoona walioko kazini ni wale wenye zamu,
tumewataka wasaini, lakini kesho hakuna atakayeingia kazini na mgomo
utakua mkali, tumekuwa wapole sana, lakini Serikali imetupuuzia,”
alisema mmoja wa madaktari.
Chama cha Tiba Asilia
Kwa
upande wa Chama cha Watabibu wa Dawa za Asili (ATME), kimewataka
madaktari kuacha kugoma na badala yake waendeleze mazungumzo na Serikali
ili waweze kufikia muafaka.
Chama hicho kupitia Mwenyekiti wake,
Abudulhaman Simba, kimesema mgomo wa madaktari unahatarisha uchumi wa
taifa na haki za wagonjwa, hasa wale wenye kipato cha chini.
Mkoa wa Mwanza
Mkoani Mwanza madaktari walio kwenye mafunzo na wale walioajiriwa waliendelea na mgomo wao jana.
Mmoja
wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa Bugando ambaye hakutaka jina
lake litajwe, alisema mgomo huo kwa sasa haujaonyesha athari kubwa
kutokana na kuwa siku za mapumziko.
"Leo (jana) na jana (juzi),
hapajatokea athari za mgomo, tunadhani athari itakuwa kubwa katika siku
za kesho (leo) na kuendelea kwani wakigoma hawa wa mafunzo na hao
wengine, kazi inakuwa kubwa kwetu," alisema.
Katika hatua nyingine, mgomo huo haukugusa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwani huduma ziliendelea kama kawaida.
Gazeti hili jana lilishuhudia wagonjwa wakipewa huduma za matibabu pamoja na mgomo uliotangazwa kudai maslahi yao.
Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Omary Chande alisema pamoja na
kutangazwa mgomo wa madaktari, Mount Meru haijaathirika na mgomo huo.
Wagonjwa waondolewa Mbeya
Katika
Hospitali ya Rufaa Mbeya, mgomo uliendelea na kusababisha baadhi ya
wagonjwa kuanza kuondolewa hospitani hapo pia na ile ya wazazi, Meta,
kwa ajili ya kwenda kutafuta matibabu kwenye hospitali nyingine za watu
binafsi.
Mwananchi jana lilishuhudia baadhi ya wagonjwa
wakipandishwa kwenye magari na kuondoka kwenda kutafuta
matibabu hospitali za watu binafsi.
Mkurugenzi wa Hospitali ya
Rufaa Mbeya, Dk Eliuter Samky alipoulizwa alikiri kuwepo kwa mgomo wa
madaktari walio kwenye mafunzo ya vitendo wanaofikia 70.
Hata
hivyo, Dk Samky alisema anao uhakika kuwa madaktari 10 bingwa
waliojariwa na Serikali wataendelea kufanya kazi, na hivyo huduma kwa
wagonjwa hasa wale walio katika hali ngumu na wale wa dharura
zitaendelea kupatikana.
Ombi la wagonjwa
Wagonjwa
jijini Tanga,wameiomba Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa madaktari ili kuondoa misunguano
iliyojitokeza.
Ombi hilo walilitoa jana walipokuwa wakizungumza
na Mwandishi wa habari hizi katika wodi za majeruhi na watoto katika
Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.
"Tunamuomba Rais atekeleze
ahadi yake aliyotoa kwa madaktari, wanapogoma sisi walalahoi ndo
tunaokufa na wengine kupata madhara zaidi, lakini wao wanapougua
wanakwenda hospitali za nje ya nchi," alisema Adamu Abdurahman
aliyelazwa katika wodi ya majeruhi ya
Galanosi.
Madaktari
waliokuwa zamu katika wodi za Hospitali hiyo walisema hawaamini kama
kweli Serikali haina fedha za kuwalipa, kwani kunapotokea masuala
mengine imekuwa ikitoa bila ya matatizo.
HUDUMA MUHIMBILI ZASUASUA
Katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, jana utoaji wa huduma kwa wagonjwa zilikuwa zikisuasua ambapo
wagonjwa walieleza hali hiyo ilianza kujitokeza tangu juzi.
Katika wodi ya watoto,
wauguzi waliokuwa wanaonekana wakifanya kazi ni wale walioitwa kwa dharura na
wengi wa madaktari hawakuonekana katika sehemu zao za kazi.
Mmoja wa daktari katika
wodi hiyo, ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema, wameamua
kusitisha huduma mpaka serikali itakaposikiliza hoja zao za msingi.
Alisema watoto wengi
wanakufa kwa ukosefu wa hewa ya oksijeni wanapofanyiwa upasuaji kutokana na
kukosekana kwa vifaa vya kuvutia hewa.
Alisema kamati iliyoundwa
na Rais Jakaya Kikwete kutatua matatizo yanayowakabili madaktari imekuwa
ikidharau vikao hivyo, na kila siku wanapokutana kunakuwa na watu wengine
tofauti na wale waliokutana nao awali.
“Kila kikao tunachokaa na
wawakilishi kutoka serikalini wanakuwa wapya, kikao hiki wanakuja hawa, kikao
kinachofuata wanakuja wengine wapya, jambo linalopelekea kutopiga hatua katika
mwafaka,” alisema daktari huyo.
Daktari huyo alisema
wanamshangaa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kwa kauli
yake ya kusema anataka kuzungumza na madaktari upya wakati anafahamu kuwa
mazungumzo na serikali yameshafanyika mara kadhaa bila ya kuafikiana madai yao.
HOSPITALI YA TEMEKE
Msimamizi Mkuu wa hospitali
hiyo, Dk. Rolesta Kinunda, alisema hakuna mgomo kwa madaktari wanaendelea na
kazi kama kawaida na wanaendelea kupokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya
jiji la Dar es Salaam.
Huduma katika hospitali
hiyo zilionekana kuendelea kama kawaida, ambapo madaktari walionekana wakipita
wodini na kutoa huduma kama kawaida.
Rashid Ndwangila, mkazi wa
Mbagala, ambaye amelazwa kwenye wodi namba saba ya wanaume hospitalini hapo
baada ya kufanyiwa operesheni ya henia alisema kwa jana madaktari walipita kama
kawaida na kuwahudumia wagonjwa wote kwa kuwapatia dawa pamoja na kuwafunga
vidonda.
AMANA NA MWANANYAMALA
Huduma katika hospitali
hizo zilionekana kuendelea kama kawaida ambapo wagonjwa walikuwa wakihudumiwa
na madaktari.
MBEYA: JAMAA WAONDOA
WAGONJWA
Baadhi ya jamaa wa wagonjwa
wameanza kuwaondoa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa ajili ya kwenda kutafuta
matibabu kwenye hospitali za watu binafsi.
NIPASHE jana liliwashuhudia
baadhi ya wagonjwa wakipandishwa kwenye magari na kuondoka kwenda
kusikojulikana.
Averine Ngeya, mzazi wa
mtoto Miliam Alex ambaye ameungua vibaya kwa maji ya moto, alisema tangu juzi
baada ya madaktari kuanza mgomo, wagonjwa hawapati huduma nzuri za matibabu
zaidi ya kupewa na wauguzi vidonge vya kutuliza maumivu.
“Tangu jana (juzi) hakuna
matibabu ya maana ambayo mwanangu ameyapata, wauguzi ndio wanatupatia panado za
kutuliza maumivu na kutuambia kuwa tusubiri daktari anaweza kuja wakati wowote,
lakini madaktari hawatokei,” alisema Ngeya.
Nipashe limetembelea katika
Hospitali ya Rufaa ya Wazazi iliyopo eneo la Meta mjini hapa na kushuhudia eneo
la hospitali likiwa halina watu kutokana na matangazo yaliyobandikwa kwenye
mbao za matangazo na kuta za hospitali hiyo yakionyesha kuwa hakuna huduma.
Ofisi za hospitali hiyo na
ile ya rufaa zilikuwa zimefungwa na wauguzi waliokuwa vibarazani walikataa
kuzungumza lolote kuhusiana na hali hiyo kwa madai kuwa wao sio wasemaji.
Mkurugenzi wa Hospitali ya
Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky, alithibitisha kuwepo kwa mgomo wa madaktari
walio kwenye mafunzo ya vitendo wanaofikia 70.
Hata hivyo, alisema anao
uhakika kuwa madaktari 10 bingwa wataendelea kufanya kazi na hivyo huduma kwa
wagonjwa hasa wale walio katika hali ngumu na wale wa dharura zitaendelea.
KCMC WAENDELEA KUGOMA
Mgomo huo umeiathiri
Hspitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, ambapo inasemekana kila idara ina
daktari mmoja wa zamu huku
wengi wakiwa kwenye mgomo.
Habari ambazo
zimethibitishwa na baadhi ya madaktari waliopo kwenye mgomo zinasema sio rahisi
kubaini athari kwa kuwa jana ilikuwa siku ya mapumziko.
“Kuanzia leo (kesho) ndio
athari za mgomo wetu zitaonekana vizuri, kwani tutaachia maeneo yote na
kubakiza eneo la wagonjwa mahututi na majeruhi wa ajali mbalimbali,” alisema
daktari mmoja na kuongeza: “Lengo si kuwaumiza wananchi bali kuishinikiza
serikali kutekeleza madai yetu.”
Mwanahamisi Ally aliyelazwa
wodi ya majeruhi na Haji Rashidi anayemuhudumia baba yake katika wodi namba
mbili, walisema huduma si za kuridhisha sana kwani kuna mabadiliko ya wazi
tangu madaktari walivyotangaza mgomo na wanaoumia zaidi ni wagonjwa, madaktari
hawaonekani wakitoa huduma na hata wakihitajiwa hawaonekani.
“Tunaiomba serikali kumaliza tatizo hili kwa haraka, sidhani kama mahakama
inaweza kuwa ndiyo suluhisho la kushinikiza madaktari warudi kazini, wakirudi
kwa mtindo huo hali haitakuwa nzuri,” alisema Rashid.
DODOMA 34 WAGOMA
Madaktari 34 walioko katika mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufani ya
Mkoa wa Dodoma, juzi hawakufika kazini licha ya kutakiwa kuwepo.
Hata hivyo, huduma katika hospitali hiyo na Kituo cha Afya cha Makole
zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezeckiel Mpuya, alisema wameendelea na
huduma za matibabu kama kawaida katika hospitali yao.
MGOMO BUGANDO WATHIBITISHWA
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza umetihibitisha baadhi
ya madaktari wake kuanza mgomo rasmi.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Japhet Gilyoma, ameliambia NIPASHE jana
kuwa, licha ya mgomo huo kuanza, lakini hali ya huduma za matibabu bado si
mbaya sana kwa sababu kuna madaktari bingwa ambao waliendelea kuhudumia
wagonjwa juzi na jana.
“Ni kweli kwamba madaktari wetu pia wameingia katika mgomo, lakini kama
unavyojua leo(jana ) ni weekend (mwisho wa juma) madaktari wanaokuwa zamu ni
wachache, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba hali ya matibabu si mbaya kwa
sababu specialists (madaktari bingwa) wanaendelea na matibabu, ” alisema.
TANGA SHWARI
Katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, jana madaktari waliokekana
wakiwa wanatoa huduma za katibabu kwa wagonjwa kama kawaida.