Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
KIJANA Emanuel Didas ambaye alifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu
katika hospitali taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (MOI),
ameishitaki Serikali akiidai fidia ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Kesi
hiyo namba 159/2012 imefunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na ndugu wa
Didas anayejulikana kwa jina la Sisti Marishay Alhamisi iliyopita baada
ya kupata idhini ya mahakama (Power of Attorney) ya kumwakilisha ndugu
yake huyo.
Katika kesi hiyo inayosubiri kupangiwa Jaji
atakayeisikiliza, Didas ameishitaki Bodi ya Wadhamini ya MOI ikiwa ni
mdaiwa wa kwanza, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akiwa
mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mdaiwa wa tatu.
Katika
hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani Marishay anadai kuwa, Oktoba
26, 2007 ndugu yake huyo alipata ajali ya pikipiki Barabara ya Bagamoyo,
jijini Dar Es Salaam na kupelekwa katika kitengo hicho (MOI).
“Alipofikishwa
hapo alilazwa na kuchukuliwa vipimo ikiwamo X-Ray na kubainika
amevunjika mfupa wa mguu wake mmoja na hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji
ili kuondoa damu iliyoganda,”anadai Marishay.
Katika hati hiyo
iliyowasilishwa mahakamani na Wakili Cornelius Kariwa kwa niaba ya mdai,
imedai kuwa Novemba mosi mwaka huo (2007), madaktari bingwa wakamfanyia
Didas upasuaji wa kichwa badala ya mguu.
Imedaiwa kuwa madaktari
hao bingwa walikiuka kanuni zote za kitabibu na utawala (SOPs) za
kufanya upasuaji kwa kuchanganya majina ya wagonjwa wakati wa kufanya
upasuaji siku hiyo.
Marishay aliyepewa idhini hiyo ya kisheria,
amedai kuwa ndugu yake alikuwa mtu aliyejiajiri kama fundi makanika na
alikuwa akiingiza kipato cha Sh25,000 kwa siku.
“Kutokana na
madhara yaliyotokana na upasuaji huo, Didas amepata hasara ya
Sh9,125,000 kwa mwaka kuanzia November 2007, hivyo anahitaji kufidiwa
fedha hizo,” amedai Marishay.
Alidai kuwa uzembe wa kiwango cha
juu katika upasuaji huo umemfanya Didas pia kuwa tegemezi akilazimika
kumuajiri msaidizi kwa mshahara wa Sh150,000 kwa mwezi kuanzia mwezi
Oktoba 2010.
Mdai katika kesi hiyo anaiomba Mahakama Kuu
kuwaamuru wadaiwa kumlipa fidia ya jumla ya Sh950 kwa kumsababishia
ulemavu wa kudumu, riba ya asilimia saba na kulipa gharama za kesi hiyo.
Pia
anaiomba mahakama kuwaamuru wadaiwa kulipa fidia maalumu ya Sh9,125,000
kwa mwaka kuanzia Novemba 2007 na Sh150,000 za mshahara wa msaidizi
kuanzia Oktoba 2010.
Kwa kiwango cha Sh9,125,000 cha fidia kwa
mwaka, kuanzia Novemba 2007 hadi Novemba 2012, Didas atakuwa anadai
fidia maalumu ya Sh45.6 milioni na misharaha ya msaidizi Sh3.1 milioni.
Didas
aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu baada ya kupata ajali lakini
akafanyiwa upasuaji wa kichwa huku mgonjwa mwingine aliyepaswa kufanyiwa
upasuaji wa kichwa akapasuliwa mguu.
Kwa sasa Didas ambaye
alifanyiwa upasuaji huo Novemba 1,2007 na madaktari bingwa wa kitengo
cha mifupa (MOI) cha hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),amepooza upande
wa kulia wa mwili wake.
Marishay alidai kuwa baada ya kuboronga
kwa madaktari hao bingwa, ndugu yake alipewa rufaa ya kwenda Hospitali
ya Indraprastha Appolo nchini India ili kujaribu kuokoa maisha yake.
Kutokana
na utata huo, MOI liunda Tume kuchunguza sakata hilo la madaktari
bingwa kuchanganya majina ya wagonjwa wawili, Didas na Emanuel Mgaya
(Marehemu), aliyepasuliwa mguu badala ya kichwa.
Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii iliikataa taarifa ya tume hiyo na kuunda tume
nyingine chini ya daktari bingwa wa mishipa ya fahamu kutoka Hospitali
ya Rufaa ya Bugando Profesa William Mhalu.
Baada ya kukamilisha
uchunguzi huo, Tume ya Profesa Mhalu ilibaini kuwa watabibu wa MOI
walikiuka kanuni zote na kuwa wazembe katika kutimiza majukumu yao siku
ya upasuaji wa Didas.
SOURCE: MWANANCHI
June 25, 2012
ALIYEPASULIWA KICHWA BADALA YA MGUU KUDAI SH BILLION 1
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget