Dk. Slaa akiwa na Rose Kamili
KATIBU
Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa, amewasilisha hoja za awali dhidi ya
utaratibu wa ufunguaji wa kesi ya kupinga ndoa aliyopanga kufunga na
mchumba wake wa siku nyingi, Josephine Mushumbusi.
Dk
Slaa na Josephine wamepanga kufunga ndoa Julai 21 wilayani Karatu
mkoani Arusha lakini juzi ilipingwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania na
mkewe, Rose Kamili.
Hoja
ya Dk Slaa iliwasilishwa jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania na wakili
wake, Mutakyamirwa Philemon. Dk Slaa katika hoja hiyo, anadai kuwa
suala la ndoa halikupaswa kuwasilishwa mahakamani kama la madai, bali
kwa kutumia hati ya kuitwa mahakamani ikiambatanishwa na kiapo cha mdai.
Kama
Kamili anayewakilishwa na wakili Joseph Tadayo atakuwa na hoja yoyote
dhidi ya hoja ya Dk Slaa, atapaswa kuiwasilisha mahakamani hapo Agosti
7. Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliahirisha kesi
hiyo hadi Agosti 14 itakapokuja kusikilizwa.
Kamili
katika kesi aliyofungua dhidi ya Dk Slaa anapinga kufungwa kwa ndoa
hiyo, na pia anadai fidia ya Sh milioni 550 kwa gharama ya malezi ya
familia na usumbufu aliopata kwa kutelekezwa na mumewe. Kesi hiyo
ilifunguliwa na Tadayo na kusajiliwa kwa namba 5 ya mwaka huu.
Kwa
mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani, mdaiwa wa kwanza ni
Dk. Slaa na wa pili ni Josephine. Kamili anadai kuwa yeye na Dk Slaa ni
wanandoa na Josephine ndiye alisababisha Dk. Slaa atelekeze familia.
Kamili
anadai yeye na Dk Slaa walifunga ndoa mwaka 1985 na Juni 18, 1987
wakajaaliwa mtoto wa kwanza wa kike Emiliana na wa pili Septemba 23,
1988 Linus na kwamba maisha yao awali yalikuwa ya upendo.
Anadai
kuwa kabla ya hapo, Dk Slaa alikuwa padri lakini kwa ridhaa yake
aliacha kazi hiyo ili aishi na familia yake na kutimiza majukumu yake
katika ndoa hiyo.
Anaendelea
kudai kuwa kuanzia hapo yeye na mdaiwa waliishi nyumba moja baada ya Dk
Slaa kuacha utumishi wa Mungu kama mke na mume na walitambuliwa kuwa
wanandoa, kwa sababu taratibu zote za ndoa zilifuatwa na familia zote
mbili ambazo zinatambua hilo.
Alitaja kuwa katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyaraka kama hati za kusafiria zinawatambulisha kama mke na mume halali.
“Mdai
na mdaiwa wa kwanza (Dk Slaa) waliishi maisha ya ndoa kwa amani, furaha
na kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya manufaa ya familia yao hapo
baadaye na walichuma mali zikiwamo nyumba ya Sinza, Dar es Salaam katika
kiwanja namba 609 Block E.
“Pia
nyumba iliyoko Karatu katika kijiji cha Gongali ambayo ilijengwa mwaka
2005 pamoja na samani mbalimbali za nyumbani,” sehemu ya hati hiyo
ilisema. Aidha, anadai mambo yalibadilika mwaka 2009 baada ya Dk Slaa
kuanza uhusiano na Josephine, na hivyo kutotimiza majukuu yake kama mume
na kulala nje ya nyumba akitumia mali za familia kutimiza maisha ya
anasa na Josephine.
“Tangu
mwaka 2009 mdai amekuwa akitunza familia peke yake bila msaada
akijitunza mwenyewe na watoto hao wawili kwa kila kitu, ikiwa ni pamoja
na ada za elimu ya juu za mtoto wa kwanza Emiliana akiwa Chuo Kikuu cha
Ardhi mwaka wa mwisho akichukua Shahada ya Usimamizi wa Ardhi na Linus
ambaye hivi karibuni amemaliza mafunzo ya Stashahada ya Tehama katika
Chuo cha Tehama cha Learn cha Dar es Salaam,” ilidai hati hiyo.
Anaiomba
Mahakama itamke kuwa ndoa inayotakiwa kufungwa Karatu au kokote na
tarehe yoyote ni batili hivyo imwamuru Dk Slaa alipe Sh milioni 50 kama
gharama ya kutunza familia kwa kipindi chote hicho na Josephine alipe Sh
milioni 500 kwa uzinzi uliosababisha mumewe atelekeze familia.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!