Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hali ya
mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatia wasiwasi na hivyo
Tanzania inafuatilia kwa makini hali inavyoendelea katika eneo hilo la nchi
hiyo jirani.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa Tanzania ingependa kuona hali ya amani inarejea katika DRC kwa
sababu nchi hiyo inahitaji kupata muda wa amani ili waelekeze nguvu zake kwenye
maendeleo badala ya kupigana.
Rais Kikwete amesema
hayo jana, Jumanne, Juni 3, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Profesa
Ntumra Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa
International Conference on Great Lakes Region (ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca
Golf mjini Bujumbura, Burundi.
Rais Kikwete
akifuatana na Mama Salma Kikwete alikuwa mjini Bujumbura kushiriki katika
Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi na kurejea nyumbani jana, 3 Juni, 2012.
Kabla ya kuja hapa, Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali, Rwanda, kushiriki katika
sherehe za namna hiyo zilizofanyika Julai Mosi, mwaka huu. Rwanda na Burundi
zilipata uhuru kutoka kwa Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2, mwaka 1962.
Rais Kikwete
amemwambia Katibu Mtendaji huyo: “ Kwa hakika hali mashariki mwa Congo inatutia
wasiwasi mkubwa na Tanzania inafuatilia kwa makini hali hiyo. Congo imekuwa
katika vita muda mrefu kupita kiasi kwa sababu tokea mwaka 1997 imekuwa katika
vita mfululizo.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Wakati umefika kwa Congo kutulia ili nguvu inayoingia katika
mapambano na vita ielekezwe katika maendeleo ya wananchi wa nchi hiyo.”
Rais Kikwete pia
ameunga mkono wazo la kuitishwa kwa mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa
ICGLR ili kujadili hali ilivyo katika mashariki mwa Congo kufuatia ombi la DRC
kutaka kuitishwa kwa mkutano huo.
Hali katika mashariki
mwa Congo imeanza kutia wasiwasi baada ya kikundi cha waasi wa Serikali ya nchi
hiyo wakiongozwa na jambazi la kivita John Bosco Ntaganda kuanza tena harakati
zake za kivita dhidi ya Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Usiku wa jana,
Jumanne, Julai 3, 2012, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
DRC,Mheshimiwa Kabila kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC. Wakati akiwa
Kigali, Rwanda,mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete pia alikutana na kufanya
mazungumzo na Rais Paul Kagame kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC.
Aidha, usiku huo huo
wa kuamkia jana, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri
Mkuu wa Ubelgiji, Mheshimiwa Didier Reynders ambaye pia anahusika na masuala ya
nchi za nje, biashara ya nje na masuala ya Umoja wa Ulaya (EU).
Katika mazungumzo Rais
Kikwete na Mheshimiwa Reynders walizungumzia hali ya mashariki mwa Congo pamoja
na mchakato wa ushirikiano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Julai, 2012