KITENDO cha Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), kusitisha usajili kwa baadhi ya madaktari waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo (Interns), kimekoleza moto wa mgomo wa madaktari baada ya wanataaluma hao kutangaza maandamano yatakayofanyika wakati wowote kuanzia sasa. Kwa muda wa wiki tatu sasa, madaktari wamekuwa katika mgomo wakitaka kuboreshewa masilahi yao na huduma za afya hospitalini, lakini wanataaluma hao walionekana kuchukizwa zaidi baada ya tukio la kutekwa, kupigwa na kutelekezwa porini kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka huku rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi akifunguliwa mashtaka ya kukiuka amri ya mahakama. Jana, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila alitaja lengo la maandamano hayo kuwa ni kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe. Dk Kabangila alitaja sababu ya pili kwamba, ni kulaani kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka cha kutekwa, kupigwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na sababu ya tatu ni kushinikiza Serikali kuunda Tume Huru ya kuchunguza suala hilo, ili wahusika wajulikane na kuchukuliwa hatua za kisheria. Alisema pia kwamba hatua hiyo imekuja kutokana na kitendo cha Serikali kuendelea kuchukua hatua ya kuwafukuza madaktari na kusitishiwa leseni wale waliokuwa chini ya mafunzo, badala ya kusikiliza na kutatua madai yao yaliyolenga kuboresha huduma hiyo nchini. “Kama mnavyofahamu, mpaka sasa takriban madaktari 400 walio chini ya usimamizi na wale walio kazini wamesitishiwa usajili na wengine kusimamishwa kazi, na haya yanaendelea wakati suala la msingi likiwa mahakamani na pia Tanzania ikiwa na upungufu mkubwa wa madaktari kwa daktari mmoja kuwa na uwiano wa kuhudumia wagonjwa 30,000,” alisema Dk Kabangila na kuongeza: “MAT inasikitishwa na dhuluma hii inayoendelea dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe na hivyo inapanga kuitisha mkutano mkubwa kesho (leo) na inatangaza maandamano ya amani ya madaktari na wale wote wenye mapenzi mema na taaluma hii na sekta ya afya kwa ujumla.” Dk Kabangila aliongeza kuwa, maandamano hayo yatafuata taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi saa 48 kabla ya kuandamana na madaktari wote watavaa makoti meupe na wasio madaktari watatakiwa kuwa na vitambaa vyeupe. Alisema maandamano hayo ya amani yataanzia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hadi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambako watakabidhi madai yao serikalini. “Tunajua tunachotakiwa kufanya ni kutoa taarifa kwa ajili ya kuhitaji ulinzi. Maandamano yetu ni ya amani na ndiyo sababu tutakuwa na makoti pamoja na vitambaa vyeupe kwa wasio madaktari, ”alisisitiza. Katika mkutano huo, Dk Kabangila alielezea kusikitishwa kwake na makundi ya watu mbalimbali na mtu mmoja, mmoja kuwatuhumu kuwa ni wauaji kwa kuendesha mgomo, akisema kitendo hicho ni hatari kwa kuwa kinawakatisha tamaa madaktari nchini. “Yameibuka makundi yanayowatuhumu madaktari kupitia vyombo vya habari, wapo wanaosema madaktari ni wauaji, hii ni hatari. Madaktari wanafanya kazi ngumu na katika mazingira magumu, hawana vitendea kazi lakini badala ya kuwafariji, watu wanajitokeza na kuwasema vibaya, sijui nini malengo yao na hatima ya taaluma ya udaktari nchini,” alisema. Alisema lengo la kushinikiza madai yao ni kutaka Serikali iweke mazingira mazuri yatakayowezesha wanataalamu hao ambao Serikali hutumia fedha nyingi kuwasomesha, kufanya kazi nchini badala ya kukimbilia nje ya nchi. Waliositishiwa usajili wanena Kwa upande wao madaktari waliokuwa katika mafunzo ya vitendo (Interns) wamelaani kitendo cha kusitishiwa leseni zao wakidai ni cha uonevu. Mwakilishi wa wanataaluma hao, Dk Frank Kagoro alilituhumu Baraza la Madaktari Tanganyika akisema limewahukumu bila kuwasikiliza, kitendo ambacho kimewanyima haki ya kujitetea. “Tumeshtakiwa kwa makosa yasiyo yetu, tumeambiwa tuwasilishe barua na tumefanya hivyo. Zile barua ilikuwa geresha, mbona hawakutuita kutuhoji? Huu ni uonevu, hata makosa waliyotuhumu nayo si makosa yetu,” alisema Dk Kagoro. Dk Kagoro alifafanua kuwa, katika barua za mashtaka kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda katika baraza hilo, madaktari hao walituhumiwa kuwa hawakutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma kwa wagonjwa, hali iliyohatarisha maisha ya wagonjwa. Akifafanua hilo, Dk Kagoro alisema tuhuma hizo siyo zao na kwamba wao wanafanya kazi chini ya madaktari bingwa, ambao wanapogoma moja kwa moja wanafunzi wanakosa kazi za kufanya. “Sisi tunafanya kazi chini ya madaktari bingwa, wao wanapogoma na sisi moja kwa moja tunakuwa hatuna kazi za kufanya, tupo kwa ajili ya kujifunza, iweje leo tuambiwe sisi ndio tuliohatarisha maisha ya watu, tungefanyaje kazi bila maelekezo ya madaktari bingwa?” alihoji Dk Kagoro. Alisema, baraza hilo limewachukulia hatua bila ya kuwasikiliza kutokana na kuwa chini ya Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambapo Mganga Mkuu wa Serikali ndiye mwenyekiti. “Kama lingekuwa baraza huru la madaktari lingetusikiliza, lakini hawa wamechukua hatua bila ya kufanya hivyo, na hii ni kutokana na kutekeleza matakwa ya Serikali, ndiyo sababu tunatarajia kujadili namna ya kuwa na Baraza Huru la Madaktari Tanganyika,” alisema. Kuhusu hatua ya kufukuzwa kazi madaktari na kusitishiwa leseni zao, alisema siyo tu inakiuka haki zao bali inahatarisha maisha ya Watanzania watakaokosa huduma za madaktari na pia kuliingizia hasara Taifa kutokana na kutumia fedha nyingi kugharimia elimu ya wanataaluma hao. “Daktari mmoja hadi anafikia hatua hii anatumia zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya kupata elimu, je, ni shilingi ngapi kwa madaktari zaidi ya 380? Haya ni mabilioni ya fedha za walipa kodi ambayo Serikali inapoteza kwa kuwafukuza madaktari,” alisema. |
Na Geofrey Nyang’oro
July 13, 2012
Madaktari waandaa maandamano
Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Millionfortune.com
JAMII
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!