Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa, amewataka wananchi kuacha tabia ya kujilimbikizia mali wakati
wakishuhudia jamii ikiangamia kwa kukosa huduma muhimu za afya, elimu
na kadhalika,“Kuna watu wamejaliwa kuwa na kila kitu, wengi hata mali
zao hawazifahamu wakati zinapopotea, lakini hayo yanafanyika wakati
kundi la jamii nyingine likiishi maisha magumu tena bila msaada, wenye
mali hawalitambui hilo,” alisema.
Askofu Malasusa aliyasema hayo
juzi jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika harambee ya
kuchangia Mfuko wa kusomesha Wanafunzi wasiokuwa na Uwezo katika Shule
ya Mtakatifu Joseph, iliyoko Mbezi Beach.
Alisema watu wanapaswa kugawana vile walivyopewa na Mwenyezi Mungu, ili kurahisisha maisha.
Mkuu
huyo wa KKKT alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba watu wenye
mali hawako tayari kugawana na wasiokuwa ma mali kama Mwenyezi Mungu
alivyofundisha.
“Mwenyezi Mungu ametufundisha kugawana kile
tunachokipata, wale wenye uwezo wawagawie wale wasiokuwa nacho, lakini
watu hawafanyi haya,” alisisitiza Dk Malasusa.
Kauli ya Askofu
Malasusa imekuja wakati kukiwa na habari kwamba Kitengo cha Polisi cha
Kimataifa (Interpol), kinachunguza Sh303.7 bilioni zinazodaiwa kukutwa
katika akaunti sita za Watanzania huko Uswisi.
Wiki
iliyopita chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Interpol kilinukuliwa na
gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, kikisema baadhi ya wanasiasa na
watu wengine nchini, ndio wanahusika na ufisadi huo.
Inadaiwa kuwa fedha hizo ziliingizwa katika akaunti hizo na kampuni za uchimbaji mafuta na madini, nchini Tanzania.
Mapema
Katibu wa Mfuko wa kusomesha watoto wasiokuwa na uwezo, Deus Valetine
alisema jamii haina hamasa ya kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu.
Alisema badala yake, hamasa ya jamii iko katika kuchangia sherehe mbalimbali za anasa.
Valetine
alisema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Event Lab kwa mwezi mmoja,
umebaini kuwa zaidi ya watu 100,000 wananga wastani wa Sh72 bilioni
kila mwaka kwa ajili ya sherehe za harusi.
“Jamii ina uratibu wa
kuchangia shughuli za jamii zilizolenga zaidi katika anasa, huku
ikishindwa kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu,”
Kwa mujibu wa Valetine harambee ya juzi, iliwezesha kukusanywa kwa Sh21 milioni .