Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema Baraza la Mawaziri
lililoundwa na Rais Jakaya Kikwete ni kubwa linalohitaji kupunguzwa ili
kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.Makamu Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Paul Lwanji alisema jana Bungeni kuwa Baraza hilo linapaswa
kupunguzwa kwa kuunganisha baadhi ya wizara na idara zinazoshabihiana
bila kuathiri utendaji wa shughuli za Serikali.
Akiwasilisha
taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais
kwa mwaka wa fedha uliopita na maoni kuhusu makadirio ya matumizi ya
mwaka 2012/2013, Lwanji alisema idadi ya mawaziri, manaibu waziri,
makatibu wakuu na manaibu wao ni mzigo mkubwa kwa walipa kodi.
Alisema
umefika wakati kwa Serikali kukubaliana na ushauri wa wadau mbalimbali
na kupunguza Baraza la Mawaziri pamoja na idara zisizo na umuhimu ili
kuendana na pato la Taifa.
“Idadi ya mawaziri 30, manaibu waziri
25, makatibu wakuu 26, Naibu Katibu wakuu 26 ni mzigo mkubwa kwa nchi
inayoendelea kama yetu. Kamati inashauri kwamba Serikali iangalie
uwezekano kupunguzwa kwa kuunganisha baadhi ya Wizara na idara
zinazoshabihiana bila kuathiri utendaji wa Serikali,” alisema Lwanji
ambaye pia ni Mbunge wa Manyoni Mashariki.
Kamati hiyo
ilipendekeza mabadiliko ya mfumo wa kuwateua watumishi wa ngazi za juu
serikalini kutokana na wengi kuonekana kutokidhi vigezo vya uongozi.
Alisema umefika wakati wa kuwekwa utaratibu na uwezo wa mtu kumudu majukumu yake na uwezo wa kiakili (IQ), sifa na uzoefu.
Alisema
katika utaratibu huo, kama mamlaka ikikosea na kumteua mtu kushika
madaraka asiyostahili au ukomo wa kufikiri ukiwa umefika mwisho, ni wazi
kuwa atashindwa kumudu nafasi yake na kuisababishia Serikali hasara.
Lwanji
alisema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikishindwa
kuwachukuliwa hatua viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Alitoa
mfano wa madiwani 1,844 ambao mwaka jana hawakuchukuliwa hatua zozote
licha ya kushindwa kutekeleza sheria ya sekretarieti, hivyo utekelezaji
wa sheria hiyo kuachwa kwa madiwani 1,032 tu.
Aliliambia Bunge
kuwa katika kipindi chote cha mwaka 2011, Sekretarieti hiyo
ilishughulikia mashauri 23 tu ya viongozi wote walioshindwa kutekeleza
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Kamati hiyo iliitaka
Serikali kutoa tamko kwa Watanzania ni lini itawafikisha mahakamani
wahusika wote waliotajwa katika ripoti ya CAG kuwa walihusika kwa namna
moja au nyingine katika kuihujumu nchi.
Kamati hiyo ilionyesha
shaka katika madai ya wafanyakazi 8,134 ambayo thamani ya madai yao
yalifikia jumla ya Sh8.3 bilioni ambayo yanaendelea kuhakikiwa na kuhoji
fedha hizo zitatoka wapi kwani hazipo katika mafungu ya bajeti.
Mishahara juu
Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kupandisha viwango vya mishahara ya watumishi wa umma kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani
alisema jana kuwa Serikali itarekebisha mishahara ya watumishi wake kwa
kuzingatia uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la
Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma.
Hata hivyo Kombani
hakuweka wazi kiwango cha nyongeza za mishahara hiyo na badala yake
alitaja fedha zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya mishahara na kulipa
madeni ambazo ni Sh3.781 trilioni.
Alisema fedha hizo
zitagharamia mishahara, upandishwaji vyeo na kulipia madai ya
malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu,
Serikali za Mitaa, Wakala na taasisi za Serikali na kwamba: “ Wenye
madai mbalimbali watalipwa madai yao.”
Kombani alisema kiasi
hicho cha fedha kimeongezeka kwa Sh510.807 bilioni ambacho ni sawa na
asilimia 15.6 ya kiasi kilichokuwa kimepangwa kutumika mwaka wa fedha
2011/2012.
“Serikali itafanya utafiti kuhusu mishahara na maslahi
ya wafanyakazi baina ya sekta binafsi na Serikali kwa lengo la
kuwianisha na kuoanisha mishahara ya watumishi wa umma,” alisema.
Alisema
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, Serikali inatarajia kuajiri
watumishi wapya 56,678 na kipaumbele kimewekwa katika sekta za elimu,
afya, kilimo na baadhi ya vyombo vya dola.
Mbali na ajira hizo, Serikali itawapandisha vyeo watumishi 42,419 ikiwa ni hatua ya kufanya maboresho katika utendaji kazi wake.
Akizungumzia
ujenzi wa kituo cha kuwaenzi waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
na Sheikh Abeid Amani Karume, alisema katika kipindi hiki cha fedha,
msingi wa jengo hilo utaanza.
Wapinzani wang’aka
Kwa
upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais na
taasisi zilizo chini yake, Profesa Kulikoyela Kahigi alizungumzia tuhuma
za rushwa zilizolitikisa Bunge.
“Zimetolewa tuhuma kadhaa na
vyombo vya habari pamoja na waheshimiwa wenyewe kutuhumiana na wengine
kukamatwa kwa tuhuma za rushwa. Ni dhahiri hata katika mchakato wa
kuchagua wabunge la Afrika ya Mashariki kauli za vitendo vya rushwa
zilitolewa na waheshimiwa wabunge,” alisema Profesa Kahigi na kuongeza:
“Kambi
ya Upinzani inaitaka Takukuru kuhakikisha kuwa pamoja na kuwakamata
watuhumiwa wengine, iendelee kuchukua hatua kulisafisha jina la Bunge
katika kashfa hii nzito inayoliondolea heshima mbele ya jamii.”
Alisema
kutokana na rushwa kuathiri maendeleo ya nchi, ni wakati mwafaka kwa
Takukuru kuwa chombo huru kiutendaji ... “Tunapendekeza uteuzi wa
Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hii ufanywe na Kamati ya Taifa ya Uteuzi na
athibitishwe na Bunge, pia taarifa za taasisi hii ziwe zinawasilishwa
bungeni kila mwaka na kujadiliwa na Bunge kama ilivyo sasa katika
kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.”