Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
PAZIA la michezo ya 34 ya taifa ya shule za msingi 'Umitashumta'
linafunguliwa leo kwa wanamichezo zaidi ya 600 kuchuana katika michezo
saba tofauti mjini Kibaha, Pwani.
Ufunguzi wa michezo hiyo
utaanza saa mbili asubuhi kwenye viwanja vya Shirika la Elimu mjini hapa
na kufunguliwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo.
Kwa mujibu wa mratibu wa wizara hiyo, Salum Salum alisema
wanafunzi hao wa shule za msingi watashindana katika michezo ya riadha,
netiboli, soka, wavu, mpira wa mikono, michezo ya walemavu
'paralimpiki' na mchezo wa bao.
"Tayari timu zimeanza kuwasili tangu wiki iliyopita na michezo hii itashirikisha Kanda 12 za bara na visiwani," alisema Salum.
Kanda
zitakazoshiriki ni Dar es Salaam, wenyeji Mashariki, Nyanda za Juu,
Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki na
Kusini.
Kanda nyingine ni Magharibi, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Ziwa
Magharibi na Kanda ya Kati ambazo kila moja itakuwa na timu ya wavulana
na wasichana.