Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
IDARA ya Uhamiaji mkoani Arusha, inamshikilia mtu mmoja anayehusishwa
na biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu waliokamatwa katika Msitu
wa Chitego, Dodoma ambapo miongoni mwao 45 walipoteza maisha kwa kukosa
hewa katika lori walilokuwemo.
Habari zilizopatikana zinaeleza
kuwa mtu huyo (jina linahifadhiwa), amekuwa akifanya biashara hiyo kwa
kusafirisha wahamiaji kutoka Ethiopia na Somalia kupitia nchini kwa muda
mrefu.
Hata hivyo, taarifa zinadai kwamba tayari kumekuwa na
njama za chini kwa chini zinazosukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya
maofisa wa idara hiyo mkoani hapa, kutaka kumwachia mtuhumiwa huyo.
Kukamatwa
kwa raia huyo kumekuja wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini,
Pereira Ame Silima akisema kwamba kitendo cha kusafirisha wahamiaji
haramu nchini kimekuwa ni mchezo wa kawaida, kwani Watanzania ndiyo
wanaowasaidia kuwasafirisha kutoka Nairobi kupitia Arusha na mara nyingi
hupita usiku katika njia za panya.
Vyanzo vya habari vimelieleza
gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa nchi jirani ya Kenya
alikamatwa Juni 25 mwaka huu wilayani Longido akiwa katika harakati za
kusafirisha wahamiaji haramu wengine kutokea nchi jirani ya Kenya.
Vyanzo
hivyo vimedai kuwa mtuhumiwa huyo mara baada ya kukamatwa alifikishwa
moja kwa moja katika makao makuu ya Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha huku
lori alilokuwa ndani yake likipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Vyanzo
hivyo, vilienda mbali zaidi na kubainisha kwamba mtuhumiwa huyo na
washirika wake wamekuwa wakilipwa Dola3,000 za Marekani kwa kila raia
wanayemsafirisha ambapo kazi hiyo imekuwa ikiwashirikisha baadhi ya
vigogo wa Idara ya Uhamiaji.
“Wamekuwa wakilipwa Dola 3,000 kwa
kila kichwa, kazi hiyo inafanywa kwa umakini mkubwa na hata maofisa wa
uhamiaji wanahusika, kwa mfano wakiwa njiani wanawasafirisha hao
wahamiaji haramu, endapo ikigundulika kwenye lori kuna mtu kafa anamweka
chini ya gari na kukanyagwa ili ijulikane aligongwa na gari kupoteza
ushahidi,” kilisema chanzo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
umebaini ya kwamba baadhi ya maofisa wa uhamiaji mkoani hapa waliwaambia
washirika wa mtuhumiwa huyo kwamba wanapaswa kutoa Sh40 milioni ili
aweze kuachiwa kitendo kilichozua mabishano makali baina ya pande mbili.
Pia
uchunguzi huo umebaini ya kwamba mara baada ya mabishano hayo washirika
hao waliomba kupunguziwa kiasi hicho cha fedha na ndipo maofisa hao wa
uhamiaji waliwaambia watoe Sh25 milioni kitendo kilichoafikiwa na pande
mbili.
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha, Daniel Namomba
alikiri taarifa za kushikiliwa kwa raia huyo na kusema kwamba
wamemshikilia akiwa na wenzake watatu.
Lakini alikanusha madai ya kutaka kuachiwa kwa njia za rushwa na kusisitiza kwamba bado wanafanya uchunguzi.
“Ni
kweli tunamshikilia, wako wanne jumla na bado tunalifanyia kazi
tukikamilisha uchunguzi tutakupeni taarifa kamili, sisi hatujabaini
chochote kuhusu tuhuma za rushwa,” alisema huku akikataa kutaja sababu
ya kukamatwa kwa raia hao.
Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini
kuwa washirika hao walikuwa na Sh20 milioni na walikuwa wakizunguka
jijini Arusha kwa kutumia gari aina ya Noah wakifanya juhudi za kujazia
Sh5 milioni ili kukamilisha kiasi chote na kukiwasilisha mbele ya
maofisa hao.
Kaimu mkuu wa idara hiyo mkoani hapa, Johannes
Msumule alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akikataa kulizungumzia
kwa undani kwa madai kwamba suala hilo ni nyeti na linashughulikiwa na
vyombo mbalimbali vya usalama nchini.
Wakati huo huo, Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa chini ya Kamanda
wake, Mbengwa Kasumambuto ameliambia gazeti hili kwamba wamejitosa
kuchunguza tukio hilo baada ya kupokea taarifa za wingu la rushwa
kutanda ndani ya sakata hilo.
July 2, 2012
Kinara wa usafirishaji wahamiaji haramu atiwa nguvuni Arusha
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget