Katika
mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa
madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu
CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake
ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika
kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini.
Nitatoa
tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa
iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa
kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya
awali kama ifuatavyo: Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu
ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania
wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa
inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa
chafu.
Mwenyekiti
wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati
hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia
madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu)
Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka
mmoja kwa mbinu mbalimbali. CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya
usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi
zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota
fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya
Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za
hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua
CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili
kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.
Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na
kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu
wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote
wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi
kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.Ni ukweli ulio wazi kwamba
CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali
katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo
michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza
kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua
kuchangia mabadiliko ya kweli.Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au
itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na
narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali,
taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea
mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.
Badala
ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya
vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao
wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa
kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta,
gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.
CCM
ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba
ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa
CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni
pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.
Ikumbukwe
kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya
uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa
ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.
Itakumbukwa
kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la
kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo
ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo
yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa
hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.
Nimeelezwa
kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni
toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai
kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani. Madai haya yaliwahi
kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na
nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na
mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na
Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni
kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.
CCM
inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora,
sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa
mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba
taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa
kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na
kuichagua CHADEMA.CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea
fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu
na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya
uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha
ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba
ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na
gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza
kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya
nchi.
Hivyo,
badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na
serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani
mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu
kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na
maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili
watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.
Hivi
karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba
serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya
ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi
watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine
na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote
kusimamia mabadiliko ya kweli.CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba
inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza
Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo
kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM
kukiri wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa
kuongoza nchi na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.
CHADEMA
tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila
masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na
makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya
CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala
hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili
ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM. CHADEMA kimekuwa chama
kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya
fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa
michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia
kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.
CCM
imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine
yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA.
Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai
ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa
mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA
toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya
uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo
alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali
kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi. Hivi karibuni, CCM
imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio
ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na
mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika
wazi kuwa ni wa kughushi.
Mikakati
yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA
inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko
nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo
CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo
watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na
kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
12/08/2012- Dodoma
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!