Wanafunzi wakivuka ziwa Nyasa kuelekea shule.
SASA
ieleweke wazi kwamba hali si shwari kati ya Tanzania na Malawi. Pengine
ni vizuri kujiuliza leo ni kwa nini mtafuruku uchukue nafasi kubwa leo.
Kivipi Mtanzania wa kawaida, aoneshwe kama ni jambo lililokuja ghafla?
Kimsingi, mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi
umekuwapo kwa zaidi ya nusu karne. Hivi sasa umechukua sura mpya baada
ya nchi hiyo jirani kusema ndiyo inayomiliki sehemu yote ya ziwa hilo.
Pengine kauli hiyo peke yake, isingeleta shari. Alama ya hatari
imetokana na kauli ya vitisho, iliyotoka Serikali ya Malawi kwamba
itafanya kila linalowezekana, ikiwamo kutumia nguvu za kijeshi
kuhakikisha ziwa hilo linabaki kwenye himaya yao.
Picha iliyopo ni kwamba Malawi wameshaona Watanzania ni wapole. Kwamba
ni waoga wa kupitiliza, kwa hiyo wakiambiwa kuhusu nguvu ya kijeshi,
watarudi nyuma. Sijui uthubutu huu wameupata wapi lakini ninachowaza ni
kwamba viongozi wa Malawi, wanahisi sisi ni mazezeta.
Vile ambavyo madai yao yalivyo hayana msingi na hayakubaliki hata
kidogo, ndivyo ambavyo ukitafakari wanachokitaka kiwe, huku wakitoa
vitisho vya kupigana vita, unaweza kujiuliza kuhusu wigo wa uelewa wao.
Ni rahisi kuamini ndugu zetu hao wana dosari za kiufahamu.
Kweli Ziwa Nyasa lote ni lao? Huo mpaka ni wa namna gani hasa, kiasi
kwamba eti Mtanzania akikanyaga tu maji ya ziwa hilo, anakuwa yupo
Malawi. Muda wa kutafuta maelewano hawataki, wanakimbilia kwenye vita.
Malawi wanahitaji kuwaheshimu Watanzania. Ni ukweli ulio wazi kuwa hii
siyo mara ya kwanza kwa Malawi kutoa madai hayo, lakini ni mara yake ya
kwanza kutumia kauli yenye vitisho vya kiwango hicho kinachoashiria vita
kati ya Tanzania na wao. Madai hayo yalitolewa kwa mara ya kwanza na
Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, Dk. Kamuzu Banda.
Madai hayohayo, yalirudiwa na wanasiasa mbalimbali, akiwemo mmoja wa
viongozi wa vyama vya upinzani, Chakufya Chiana. Baadhi ya maswali
yanayoulizwa ni haya yafuatayo;
Je, ni mambo yapi yameshindikana kutatuliwa katika mgogoro huo kwa muda
wote huo wakati kuna vyombo vya kimataifa vyenye uwezo na mamlaka za
kusuluhisha migogoro kama hiyo? Pili, ni upande upi ambao umeonekana
kukwamisha mazungumzo hayo?
Kwa muda mrefu yamekuwapo mazungumzo kuhusu mgogoro wa mpaka huo,
kupanuka kwa mgogoro huo hivi sasa kumechochewa na dalili za kuwapo kwa
kiasi kikubwa cha gesi na mafuta katika ziwa hilo na hatua ya Malawi
kuingia mkataba na kampuni ya Surestream Petroleum ya Uingereza.
Kampuni hiyo, tayari imeanza utafiti na utafutaji wa nishati hiyo,
ikiwamo sehemu za eneo la Tanzania katika ziwa hilo. Kauli ya shari ya
Serikali ya Malawi ilitokana na hatua ya Serikali ya Tanzania kuitaka
serikali hiyo kusitisha shughuli hizo hadi suala la mpaka litakapopatiwa
ufumbuzi.
Je, baadhi ya mambo kwenye mgogoro yamekuwa yakifanywa siri? Mbona sasa
hali ya amani imehatarishwa hivi sasa? Ukweli ni kwamba Tanzania na
Malawi, zimekuwa na uhusiano mzuri kiasi cha wananchi wa pande zote
katika mpaka huo kutembeleana, kuoana, kufanya biashara na hata kupata
huduma zote pasipo kujali uraia wao. Mtazamo wangu unanifikisha kwenye
jawabu kwamba endapo wananchi wa pande zote mbili wangejua nani amekuwa
kikwazo katika juhudi za kutatua mgogoro huo, wangeweka shinikizo kwa
viongozi wa pande hizo mbili na hatimaye kupata suluhu ya mgogoro huo.
Kwa kuangalia sura ya undugu uliopo kati ya Watanzania na Wamalawi, kwa
hakika vita haitakiwi. Lakini tunafanyaje ikiwa ndugu zetu hao wanataka
mapambano? Je, vita ni utashi wao au Malawi inatumiwa ili kutia dosari
historia yetu nzuri, kwamba ni kisiwa cha amani? Muda utaeleza.
Watanzania hatutakiwi kuombea vita kwa sababu hiyo siyo sherehe. Kwamba
watu watakutana ukumbini, kucheza muziki, kula kuku, bata, kunywa supu
na aina nyingine ya maakuli. Tukumbuke Vita ya Kagera iliyomwondoa Nduli
Iddi Amin.
Vita hiyo kama mfano hai kabla ya kuingia kwenye vita na Malawi,
iliigharimu Tanzania maisha ya watu na kubwa zaidi ni mali. Tanzania
ilipata hasara ya fedha za kigeni zaidi ya shilingi trilioni 5. Wananchi
wa leo, waliokuwa na akili timamu kwa wakati huo, wanakumbuka madhara
makubwa yaliyotokea.
Kama ni ushauri, basi napendekeza kwamba mgogoro huo wa mpaka kati yetu
na Malawi umalizike kwa pande zote mbili kufikia maridhiano badala ya
vita. Lakini kama hawataki je? Na kwa nini watangulize kauli ya kutaka
vita? Kama si tamaa ya mafuta na gesi, basi wametumwa kuvuruga amani
yetu.
Kwa upande mwingine, Malawi haiwezi kulaumiwa kwa sababu mgogoro huo ni
pandikizi la ukoloni uliotokana na mkataba wa mwaka 1890 ambao
ulielekeza kwamba sehemu yote ya ziwa hilo iwe upande wa Malawi. Hata
hivyo, swali la kujiuliza ni hili; Je, viongozi wa Malawi, wao hawatumii
akili?
Kweli Ziwa Nyasa lote ni lao na Tanzania haina eneo kabisa? Tanzania
inayo haki ya kumiliki nusu ya eneo la ziwa hilo kutokana na Mkataba wa
Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari ya mwaka 1982 inayotaka nchi
zinazogawana eneo la bahari au ziwa zigawane eneo hilo nusu kwa nusu.
Chanzo: GPL
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!