Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Ndugu zangu,
Ahsanteni kwa mitazamo yenu. Katika hili yawezekana tukawa na mitazamo tofauti, ni hali ya kibinadamu. Kwangu mimi, kwa wanahabari huu si wakati wa kutangaza mgomo wa kuripoti habari za kipolisi, kinyume chake, ni wakati wa kushambulia kwa pamoja kwa kuwakabili polisi na wahusika wengine kwa maswali yenye kuhitaji majibu.
Huu ni wakati wa jeshi la wanahabari kuishambualia polisi kama taasisi muhimu ya dola ili ipate majibu ya maswali ambayo jamii inataka majibu yake. Mbali ya tukio la mauaji ya mwandishi mwenzetu Daud Mwangosi, hatuwezi kuacha kufanya kazi na polisi kupata majibu ya matukio mengine ya kihalifu yanayotokea katika jamii kwa vile tu tuna mgogoro na polisi.
Naamini, tofauti na kugoma, kuna njia nyingine za kuishinikiza Serikali na hata taasisi ya polisi kuchukua hatua katika yanayotokea. Na moja ya njia hiyo ni kila linapotokea tukio, kwa wanahabari kwa uwingi wetu, ' kuvamia' ofisi za wenye kuhusika na kutoa majibu ya maswali ambayo jamii inataka majibu yake.
Msimamo wangu huu unaeleweka hata na baadhi ya viongozi wa juu wa Iringa Press Club ambao nina ushirikiano nao mzuri. Na jema katika hili ni kuwa, ushauri wangu wa namna ya kwenda mbele umepokelewa vema na Makamu Mwenyekiti ( Francis Godwin) na Katibu Mkuu wa IPC ( Frank Leonard) ambao kimsingi nimefanya mazungumzo nao na wanaufanyia kazi ushauri wangu.
Vinginevyo, naelewa hasira na jazba tuliyo nayo wanahabari wengi kutokana na kilichotokea. Hata hivyo, hata katika hali kama hii, tuwe na ujasiri wa kumeza vipande vya barafu. Tutangulize hekima na busara. Ndio, tutulie na kupanga mikakati ya pamoja itakayohakikisha jamii tunayoitumikia hainyimwi haki yake ya kimsingi ya kupata habari ikiwamo habari za kipolisi. Na hata katika hili, jamii ina mengi inayoyahoji kupitia wanahabari. Wenye kuhitajika kuhojiwa ndio hao tunaofikiria kuwagomea. Naam, tuna lazima ya kuwahoji wahusika. Ni kazi yetu.
Ndio, mikakati hiyo ituhakikishie wenye kuhusika na kutoa majibu ya unyama uliomtokea mwanahabari mwenzetu hawapati muda wa kupumua. Hii ni pamoja na sisi tulio mstari wa mbele kuhakikisha kila kukicha wahusika wanatukuta nje ya milango ya ofisi zao tukisubiri majibu ya maswali ambayo jamii inayauliza.
Kwamba matukio kama ya mauaji ya Daud Mwangosi kamwe yasiwe ni ' Upepo tu unaopita'- Kwa wanahabari kugomea kuwakabili polisi kwa maswali ni namna moja au nyingine ya kutengeneza mazingira ya kuruhusu ' Upepo upite'.
Kufanya hivyo ni kulisaliti jukumu letu la msingi- Kuitumikia Jamii ya Watanzania.
Na Mpiganaji Maggid Mjengwa
September 6, 2012
JE, WAANDISHI KUGOMEA HABARI ZA KIPOLISI, MAONI YAO YAPO VIPI? HAYA NDIO MAONI YA MAJJID MJENGWA
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!