Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema lazima Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ianze Septemba 15 kama ilivyopangwa hata kama makubaliano na wadhamini wa ligi hiyo yatakuwa hayajafikiwa.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa ligi hiyo haitaanza katika tarehe iliyopangwa kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kutofikiwa kwa maafikiano baina ya TFF na wadhamini wa ligi hiyo, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya TFF, Wallance Karia, alisema kuwa kamati haiko tayari kubadilisha ratiba ya kuanza kwa michuano ya ligi hata wasipokubaliana na wadhamini kwa wakati kwavile maandalizi mengine yote yamekamilika.
Karia aliongeza kuwa hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na wadhamini.
“Tunatarajia kusaini mkataba mpya na Vodacom ndani ya wiki hii. Ligi Kuu lazima ianze Septemba 15 kama inavyoonesha kwenye ratiba. Hakuna kitu kitakachotukwamisha,” aliema Karia.
“Kila timu inayoshiriki ligi msimu huu ina mdhamini wake. Tunaona hata kabla ya kuanza kwa ligi, timu zinasafiri zenyewe na kucheza mechi za kirafiki… hatuwezi kusubiri pesa za wadhamini wakuu ndipo ligi ianze,” aliongeza.
Udhamini wa awali wa Vodacom kwa ligi hiyo ulifikia tamati yake ya miaka mitano Agosti 31.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!