StatsCrop - Free website analyzer!

Ads 468x60px

AddToAny

Lorem

Social Icons

September 6, 2012

TUNDU LISSU: TUME YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA DAUD MWANGOSI IMEUNDWA KINYUME CHA SHERIA

Tweeted this Like this, be the first of your Friends

Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (kushoto), 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kutounga mkono tume ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, mkoani Iringa, kwa madai kwamba, imeundwa kinyume cha Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 1962 Sura ya 29.


Kimesema kwa mujibu wa sheria hiyo, tume zote za uchunguzi huundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye huzipa pia hadidu za rejea na baadaye kutoa ripoti kwake au hadharani endapo ataelekeza hivyo katika hadidu za rejea atakazoipa na haziundwi na waziri.

Tume hiyo, ambayo inahusisha wajumbe kutoka tasnia za sheria, habari, Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), iliundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa nia ya kupata matokeo yasiyoegemea upande wowote.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, wajumbe ni Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications; Ofisa Mipango wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike; mtaalamu wa milipuko kutoka JWT, Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu.
Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa alisema tume hiyo haina lengo la kuchunguza mauaji, bali kurekebisha uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari.
“Kwa hiyo, si tume ya kuchunguza mauaji, ni tume ya kurekebisha mambo, ku-repair hii public relations dizasta iliyotokea tarehe 2 juzi ya Jeshi la Polisi kukamatwa mchana kweupe ikiua mwandishi wa habari. Kwa hiyo, ni tume ambayo lengo lake…ni kuondoa hii picha ya mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi hadharani kwenye vichwa mbele vya magazeti. Hivyo ndivyo tunavyoiangalia sisi,” alisema Tundu.
Alisema kwa kuwa tume hiyo si ya kuchunguza mauaji, Chadema haitaiunga mkono na pia itawashauri Watanzania, wawe wanachama wa chama hicho au la kutoiunga mkono.
Lissu alisema hawaungi mkono tume hiyo kwa sababu masuala ya kuunda tume za uchunguzi wa mambo yanayotokea kitaifa ni jukumu kisheria la Rais na siyo la waziri, ambaye anaowasimamia ndiyo watuhumiwa wa kile kinachotakiwa kuchunguzwa.
Alisema kwa upeo huo wa kisheria, Waziri Nchimbi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji yaliyofanywa dhidi ya mwandishi huyo wa habari na Jeshi la Polisi analolisimamia.
Lissu alisema walioua ni Jeshi la Polisi, hivyo inawezekana polisi waliamriwa kuua na wakuu wao katika jeshi au wakuu wao kisiasa.
Alisema wakuu wa jeshi hilo katika mamlaka ya kisiasa ni waziri na mkuu wao wa juu kabisa katika mamlaka ya kiutendaji, ni Inspekta Jenerali (IGP).  
Alisema kinachochunguzwa ni mauaji yaliyotokea waziwazi, inawezekana yalifanywa kwa amri za wanasiasa kwa maana mamlaka ya kisiasa inayosimamia Jeshi la Polisi au yaliamriwa na Mkuu wa Jeshi hilo au maofisa wake wengine wa ngazi ya juu.
“Sasa hii tume inayoundwa na waziri yenye wateule wa waziri ina uwezo wa kumhoji waziri kuona kama anahusika au hahusiki? Je, tume, ambayo mmoja wa wajumbe wake ni Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, inaweza ikamwita IGP Mwema? IGP anaweza akaamriwa na wale wa chini yake kina Mngulu kwenda kutoa ushahidi mbele ya tume hiyo? Kiutendaji haiwezekani,” alisema Lissu na kuongeza:
“Ndio maana waliotunga Sheria ya Tume za Uchunguzi walisema mamlaka ya kuunda tume za uchunguzi ni mamlaka ya Rais. Kwa sababu tume ikiundwa kwa mamlaka hayo inakuwa ina-act kwa jina la Rais. Inakuwa inafanya wajibu wake kutokana na mamlaka ya Rais. Kwa hiyo ukiitwa hata na Mngulu wewe kama IGP au kama waziri unaitwa kwa sababu wanaokuita wamepata mamlaka ya Rais.”
Lissu alisema sababu nyingine za kutounga mkono tume hiyo, ni kuongozwa na Jaji Ihema, ambaye alisema rekodi ya utendaji wake wa kazi hawaiamini.
Alisema pia wajumbe wenzake (Jaji Ihema), kama vile Mngulu, naye hafai kuwamo kwenye tume kwa sababu hawezi kumwita bosi wake, IGP Mwema ili kumhoji iwapo amri ya kuua ilitoka kwake, pia hawezi kumwita Waziri Nchimbi ili kumhoji kama aliliamuru Jeshi la Polisi kuishughulikia Chadema, kama lilivyoua mkoani Arusha, Morogoro na sasa Iringa.
Pia alisema hawaoni mantiki katika tume hiyo kuwapo mtaalamu wa milipuko, kwa sababu hakuna anachokwenda kuchunguza, kwani picha za magazeti na zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilizotoka muda mfupi baada ya mauaji ya mwandishi, silaha iliyotumika, ambayo ni ya kurushia maguruneti ya moshi inajulikana.
Kuhusu Makunga na Mtambalike, alisema hao ni waandishi wa habari na kuhoji: “Wana utaalamu wa kuchunguza vifo?” 
Aliishangaa hadidu rejea ya kwanza ya tume, ambayo ni kuchunguza chanzo cha kifo na kuhoji: “Nani miongoni mwenu, ambaye hajui chanzo cha kifo cha marehemu Daudi Mwangosi…? Kama chanzo kinajulikana kwa sisi tusiokuwa wataalamu, hawa wataalamu wanakwenda kuchunguza chanzo kipi kingine?”
Kuhusu hadidu rejea nyingine ya tume, ambayo ni kuchunguza uhasama wa polisi na vyombo vya habari, Lissu alisema haijulikani kama kinachochunguzwa ni mauaji au sababu za polisi kugombana na vyombo vya habari na kuhoji: “Hiyo ni nini?”.
Kuhusu hadidu rejea nyingine, ambayo ni kuchunguza nguvu iliyotumika katika tukio lile kama ilikuwa kubwa kupita kiasi, alisema suala hilo ni la kisheria na la ushahidi na si la uchunguzi.
Kuhusu hadidu rejea nyingine ya kuchunguza uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa, Lissu alisema hajawahi kusikia jeshi hilo limevunja maandamano au mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) au mikutano inayoendelea hivi sasa katika Jimbo la Bububu.
Hivyo, akasema kinachoenda kuchunguzwa na tume hiyo si uhusiano kati ya jeshi hilo na vyama hivyo, bali kati ya jeshi na Chadema, kwani mikutano yake ndiyo, ambayo imekuwa ama inashambuliwa na watu kuuawa au inapigwa marufuku na polisi.
Alihoji sababu za Mngulu kuwamo kwenye hiyo tume na kutokuwapo kwa watu wa Chadema, Msajili wa Vyama vya Siasa au mjumbe kutoka ofisi yake. 
Unachunguza mahusiano ya polisi na vyama vya siasa au unataka kutengeneza ripoti itakayosema Chadema walikosea, Jeshi la Polisi walikuwa sawasawa kufanya walichofanya? Hii siyo tume ya uchunguzi, hii ni tume ya kufunika mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi…Kwa sababu hiyo hatuwezi kukubaliana na tume ya Nchimbi,” alisema Lissu.
Alisema wanahitaji uchunguzi ufanyike si kwa tukio la Iringa tu, bali kwa matukio mengine yote ya mauaji, yakiwamo ya watu watatu Arusha, mwanachama wa Chadema wilayani Igunga, kiongozi wa Chadema aliyeuawa kwa kuchinjwa baada ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki na ya mwananchi aliyeuawa mkoani Morogoro.
Alisema wanachotaka ni kwamba, badala ya tume hiyo iundwe Tume ya Uchunguzi ya Kijaji itakayoongozwa na majaji wanaofahamika kwa uadilifu, utendaji wao wa kazi na kutokuwa na doa katika uteuzi wao.
Alisema majaji hao wawe wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania au wachanganyike na wa Mahakama Kuu, ambao hawana madoa watakaofanya uchunguzi wa wazi utakaofanyika hadharani.
Lissu alisema katika uchunguzi huo, mashahidi wataitwa na tume, na ushahidi wao utatolewa hadharani, watahojiwa na mawakili wa tume hadharani, pia watahojiwa na mawakili wa familia za wote walioathirika hadharani na ripoti itatoka hadharani.
Alisema tume za aina hiyo hapa nchini hazipo, lakini kwa mujibu wa sheria hiyo, Rais anaweza akaianzisha na kuipa mamlaka hayo na hadidu za rejea za kuchunguza mambo hayo hadharani.
Alisisitiza Chadema haitaki uchunguzi wa kificho, kwa sababu utaleta majibu kwamba, polisi hawakukosea kama walivyosema katika tukio la Morogoro na kama, ambavyo alivyopigwa wilayani Tarime, ambako polisi waliua, wakasema watafanya uchunguzi, lakini mpaka leo haijulikani kama ulifanyika au la. 
Alisema tume hiyo ya majaji itakuwa na mamlaka ya kumwita mtu yoyote, akiwamo Waziri Nchimbi na IGP Mwema, isipokuwa Rais kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi.
Pia alisema wanataka maaskari wote waliokuwapo katika matukio ya Iringa, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka ya mauaji, kwani pamoja na kwamba, si wote walifyatua bomu lililomuua Mwangosi, katika sheria ya jinai, maaskari hao, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Michael Kamuhanda, wanahesabika kuwa walikuwa na lengo la pamoja la kuua.
Vilevile, alisema Waziri Nchimbi ajiuzulu kama alivyofanya Waziri mwenzake katika wizara yake, Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1976, baada ya Jeshi la Polisi kutesa na kuuawa watu mkoani Shinyanga, na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Zanzibar, Hamad Masoud, aliyejiuzulu baada ya meli ya MV Skagit kuzama na kuua watu.
Alisema Dk. Nchimbi hawezi kuendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kuheshimiwa kama waziri kwa sababu jeshi analolisimamia ni wauaji.
MADAI YA NAPE
Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye, amedai mauaji dhidi ya Mwangosi yamesababishwa na hatua ya Chadema kukaidi amri halali ya polisi ya kuwataka kusitisha mikutano ya hadhara hadi sensa ya watu na makazi itakapomalizika.
Hivyo, akataka viongozi wake kuwajibika si kwa mauaji hayo tu, bali pia kwa mengine yaliyotokea mkoani Singida na Morogoro katika shughuli za kisiasa za chama hicho.
Hata hivyo, Nape alisema aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, alisema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwangosi na kujeruhiwa kwa askari watatu katika tukio hilo.
TENDWA ATISHIA KUFUTA VYAMA
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amesema sasa atakifuta chama chochote kitakachosababisha mtu kupoteza maisha, kutokana na mikutano yake ya kisiasa kama iliyotokea Iringa kwa kuwa sheria inamruhusu kufanya hivyo.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kukataa kuendelea kuruhusu raia kufa kutokana na mikutano ya kisiasa na akaviasa vyama na Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wa kila upande, kwa mujibu wa Sheria ya Mikutano ya Vyama vya Siasa, Ibara ya 11.
“Ni muhimu tukajiuliza kama mwenendo wa chama fulani cha siasa inakidhi matakwa ya sheria hii ya mikutano au la. Sheria ina vifungu vya kutekelezwa na vyama pale vinapotaka kufanya mikutano yake, lakini pia inaelekeza wajibu wa jeshi la polisi kuhusiana na mikutano hiyo,” alisema.
Alisema ofisi yake ilianza kushuhudia matukio ya mauaji yanayotokana na mikutano ya kisiasa tangu mwaka jana, Arusha, na baadaye Singida, Morogoro na majuzi Iringa, kwa sababu ya kukiukwa sheria hiyo, katika kipindi chote cha miaka 12 aliyokaa katika ofisi hiyo.
Tendwa alisema atafuta chama chochote cha siasa kitakachosababisha kifo cha mtu bila kujali kama kina wabunge au la na bila ya kujali kuwa, kutakuwa na chaguzi ndogo nyingine kwa kuwa maisha ya watu ni muhimu, kuliko kazi ya kufuta chama au kuingia gharama ya chaguzi nyingine.
DCI MANUMBA ASHIKWA NA KIGUGUMIZI
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, jana alishikwa na kigugumizi kutoa taarifa ya awali ya uchunguzi ya mauaji ya Mwangosi  baada waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa kumtaka awatoe polisi wa mkoa huo katika chumba cha mazungumzo.
Waandishi walimweleza katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, kuwa hawatakuwa tayari kupokea taarifa yoyote kutoka kwa Manumba endapo maofisa polisi wanaofanya kazi mkoani humo wataruhusiwa kushiriki mkutano huo.
Manumba alisema jana alitaka kuwapa waandishi taarifa ya uchunguzi ya mauaji hayo uliofanywa na timu iliyoundwa na Jeshi la Polisi, lakini ameshindwa kuwapa kutokana na sharti walolimpa.
Alisema kila mtu ameguswa na mauaji ya mwandishi huyo na kwamba, kosa lililofanywa na wahusika haliwezi kuwa kosa la kila mtu.
 “Kwa kuwa huu ni msimamo wa waandishi na wote mmeuunga mkono mbele yangu, nadhani uchunguzi uliofanywa na jeshi letu itabidi upitiwe na tume nyingine badala ya kuutoa kwenu,” alisema.
Alisema tume iliyoundwa na Waziri Nchimbi inatakiwa iachwe ifanye kazi yake na kwamba itapata fursa pia ya kupitia uchunguzi wao huo.
Manumba alisema katika kipindi hiki kigumu kwa wanahabari na wadau wa tasnia hiyo, yapo mengi yatakayozungumzwa kuhusu kifo cha Mwangosi, zikiwamo taarifa za uzushi, za kupikwa na za ukweli.
Imeandikwa na Muhibu Said na Raphael Kibiriti Dar; George Ramadhan Mwanza; na Vicky Macha Iringa.

0 comments:

Post a Comment

Toa maoni yako hapa!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
Web Directories
PageHeat