INADAIWA kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari tukio hilo limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha tukio hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani Mbeya.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa polisi hao kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa mbalimbali likiwamo gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla ya mkutano huo wa Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali, hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”
Askari mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate (malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza kwamba, askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka mjini Dodoma.
Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
Makamanda watupiana mpira
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakukubali wala kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo yanatakiwa kujibiwa na Kamanda wa Iringa.”
Aidha, alisema sakata la kifo cha mwandishi huyo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi hivyo asingekuwa tayari kulizungumzia.
“Siwezi kusema kama askari wangu walikwenda huko au hawakwenda, isipokuwa ninachoweza kusema ni kwamba suala hilo lipo katika vyombo husika hivyo waachiwe wao au Kamanda wa Iringa ndiye mwenye majibu.”
Alipotajiwa jina la mmoja wa askari aliyeonekana katika picha za video na magazeti za tukio hilo kwamba anatokea katika moja ya vituo vyake, kamanda huyo alisema: “Mimi yakitokea Dodoma nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa hiyo, mambo ya Iringa siwezi kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda kuzungumza jambo hilo hamuoni kuwa itakuwa ni kama vurugu?”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka askari wake Iringa akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari yeyote aliyekwenda Iringa wakati wa vurugu zile.”
Mkutano wa DCI wavunjika
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema: “Hayo yote yameundiwa tume ngoja tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali, DCI Manumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani Iringa, ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya kutokea kutoelewana baina yao.
Manumba alitaka kueleza ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini waandishi hao walikataa kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo kwa kuwa ulifanywa na polisi peke yao.
Kabla Manumba, hajaanza kuzungumza, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC), Frank Leonard alisema kutokana na msimamo wa waandishi wa habari wa mkoa huo hakutakuwa na uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale tume zilizoundwa kuchunguza kifo hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya mauaji hayo.
“Msimamo wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.
Akijibu madai hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja kulizungumza.”
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
Chanzo Mwananchi
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!