Mshindi wa EBSS, Walter Chilambo
MSHINDI wa Shindano la kumtafuta msanii mwenye kipaji cha muziki maarufu kama Epiq Bongo Star Search (EBSS) hatimaye amejulikana usiku huu ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee. Aliyefanikiwa kushinda taji hilo mwaka huu ni msanii chipukizi mwenye kipaji cha muziki na sauti laini Walter Chilambo, ambaye tayari amekabidhiwa kitita cha sh. milioni 50 za Kitanzania usiku huu.
Chilambo ameibuka mshindi baada ya kumshinda mshiriki Salma Abushir kutoka Zanzibar, ambaye ameshika nafasi ya pili. Mshindi wa tatu katika shindano hilo ni Wababa Mtuka aliyeenguliwa katika hatua ya tatu bora kabla ya kusalia washiriki wawili. Washiriki waliofanikiwa kuingia fainali ya shindano hilo ni watano, ambapo ni Nshoma Ng’hangasamala, Walter Chilambo, Wababa Mtuka, Nsami Nkwabi na Salma Abushir.
Mashindano hayo yamesindikizwa na wasanii anuai maarufu wa nchini kama vile Rich Mavoko, Omi Dimpoz, Ben Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto, Laila Rashid, Linex pamoja na Barnaba.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!