Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Kaskazini ya Dk Martin Shao amewasihi madaktari waliogoma katika
hospitali mbalimbali nchini ikiwamo KCMC kurejea kazini.
Hospitali
ya Rufaa ya KCMC inayoendeshwa na Shirika la Kidini la Msamaria Mwema
(GSF) la KKKT ni miongoni mwa hospitali zilizokumbwa na mgomo ulioanza
Jumatatu wiki hii.
Akizungumza na gazeti hili jana, Askofu Shao
alisema kuwa hata ikiwa madaktari hao wana hoja za msingi kiasi gani,
zinaweza kupoteza ushawishi iwapo watatumia njia zisizo halali
kushinikiza madai yao.
“Walitakiwa kuwa waungwana, walipaswa kujua
wito wao kwa maana ya maisha ya wagonjwa kwanza maslahi baadaye. Njia
bora ya kutatua migogoro ni mazungumzo, ”alisema Askofu Shao.
Askofu
Shao alisema anazo taarifa za madaktari walio katika mafunzo kwa
vitendo katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya KCMC kuingia katika mgomo
lakini, akasema suala lao linashughulikiwa na Serikali.
“Hili la
madaktari walio mafunzoni tunashukuru linaendelea kutufanyiwa kazi na
Serikali, hata mahakama imetoa amri yake, nawashukuru madaktari bingwa
na wanaosomea ubingwa wako kazini,”alisema.
Hali ya utoaji huduma
katika hospitali hiyo imezidi kuzorota baada ya madaktari wanaofikia 80
kugoma kurejea kazini huku taarifa zikieleza kuwa hadi jana walikuwa
hawajarejea kazini.
Baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamepewa rufaa
kutoka hospitali mbalimbali kwenda KCMC, walijikuta wakirudishwa
walikotoka kutokana na mgomo huo unaoendelea.
Mbali na
kutopokelewa kwa wagonjwa wapya wanaohitaji kulazwa, kliniki zote za
wagonjwa wa kisukari, Ukimwi na waliofanyiwa operesheni zimefungwa rasmi
kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mgomo wa madaktari ulianza mwanzoni
mwa wiki hii wakidai kutotekelezwa kwa madai yao ya maslahi bora kama
walivyoahidiwa na Serikali kupitia vikao vya upatatishi, hata hivyo
Serikali imepeleka suala hilo mahakama ya kazi kutafuta ufumbuzi ambapo
leo itatoa tamko bungeni.