Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru upande wa mashtaka kumpa
aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL), Theophil Makunga na wenzake wawili maelezo ya
malalamikaji ili waweze kufahamu zaidi kuhusu kesi yao.
Makunga
anakabiliwa na shtaka la kuchapisha makala ya kuwashawishi askari na
maofisa wa majeshi nchini kuacha kuitii Serikali. Uamuzi huo ulitolewa
jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema baada ya Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Elizabeth Kaganda kumaliza kuwasomea maelezo ya awali
washtakiwa. Wakili wa utetezi, Gabriel Mnyele aliiomba mahakama hiyo
iuamuru upande wa mashtaka kuwapa washtakiwa hao maelezo ya
malalamikaji ili yaweze kuwasaidia kuifahamu vizuri kesi
inayowakabili.
Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda alidai kuwa hana pingamizi na
ombi hilo na kwamba atawapatia. Akitoa uamuzi juu ya ombi hilo, Hakimu
Lema aliutaka upande wa mashtaka umpatie kila mshtakiwa maelezo ya
mlalamikaji na kwamba dhamana zao zinaendelea.
Awali akiwasomea
maelezo hayo, Kaganda alidai kuwa Makunga ambaye ni Mhariri Mtendaji
Mkuu wa MCL akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji, Novemba 30, 2011
alichapisha waraka wenye kichwa cha habari 'Waraka Maalumu kwa askari
wote', ambao uliandikwa na Samson Mwigamba kwenye gazeti la Tanzania
Daima toleo la 2553. Kaganda alidai Makunga alifanya kosa hilo kinyume
na kifungu cha 32 (1) (c) na 31 (1) (a) cha Sheria ya Magazeti sura ya
229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akiendelea kuyasoma
maelezo hayo ya awali, alidai kuwa Samson Mwigamba na Abisalom
waliwashawishi askari na maofisa wa Jeshi la Polisi, Magereza pamoja na
Jeshi la Ulinzi la Wananchi nchini (JWTZ), kutoitii Serikali jambo
ambalo ni kinyume na kifungu cha 46(b), 55(10(a) na 35 cha Sheria ya
Kanuni ya Adhabu kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa
Novemba 30, 2011, gazeti la Tanzania Daima, toleo namba. 2553
lililochini ya Kibanda (Mhariri Mtendaji), lilichapisha waraka huo ambao
uliandikwa na Samson Mwigamba kupitia safu yake ijulikanayo ‘Kalamu ya
Mwigamba’.
Baada ya Kaganda kusoma maelezo hayo ya awali,
ambayo washtakiwa wote waliyakana na kukubali vyeo na majina yao pekee.
Kaganda aliieleza mahakama kuwa wao watapeleka vielelezo vitatu
ambavyo ni maelezo ya onyo waliyoyatoa washtakiwa polisi, gazeti
lililoandika walaka huo unaodaiwa kuwa ni wa uchochezi na maoni ya
wataalam.
Hakimu Lema aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7 ,
mwaka huu itakapoanza kusikilizwa. Makunga alikaimu nafasi ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi (MCL) kwa zaidi ya miezi
mitano baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Sam Shollei
kumaliza muda wake. Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Tido Mhando.
Awali
Machi 26, mwaka huu, kwa mara ya kwanza alisomewa shtaka hilo
linalomkabili. Makunga anatetewa na Mawakili Mabere Marando na Frank
Mwalongo. Makunga aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya
dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh5 milioni,
mmoja wa wadhamini hao atoe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya
kiasi hicho cha fedha na kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani,
kuripoti polisi mara moja kila mwezi na kutotoka nje ya Dar es Salaam
bila ya kibali cha mahakama.
Februari 15, mwaka huu, Wakili huyo Mwandamizi wa Serikali aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Chanzo: Mwananchi