Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea,
Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth
Michael (Lulu) anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven
Kanumba. Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke
Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa
pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais
Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam. De-Mello ni miongoni mwa
mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi
hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu. Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.
Akizungumza
kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa
Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana
na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Majaji
wengine walioapishwa jana na Rais Kikwete ni Francis Mutungi, John
Mgeta, Patricia Fikirini, Sam Rumanyika, Salvatory Bongole, Jerald
Alex, Mathew Mwaim, Jacob Mwambegele na Latifa Mansook. Jaji Mkuu,
Mohamed Chande Othman alisema amefurahi kuteuliwa kwa majaji hao na
anawafahamu kuwa wote ni wazoefu na watatekeleza kazi zao kikamilifu. “Wote
ni wazoefu. Ukiangalia utaona kuwa sita walikuwa wakifanya kazi
mahakamani (Mahakama Kuu na Rufani), wawili mawakili wa kujitegemea na
wawili pia mawakili wa Serikali,” alisema Jaji Othman.
Alisema
majaji hao wote kabla ya kupangiwa kazi rasmi itabidi waanze kufanya
kazi ya kukabiliana na kesi zaidi ya 2,200 zilizopo katika Mahakama Kuu
kitengo cha Ardhi.
Uteuzi wa majaji hao 10, alisema unaifanya Mahakama Kuu sasa kuwa nao 69 tofauti na wale 16 wanaounda Mahakama ya Rufani. Othman alisema pamoja na uteuzi huo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kulundikana kwa kesi nyingi kuliko uwezo wao.
“Walioteuliwa watasaidia lakini ukweli ni kwamba bado tunakabiliwa na upungufu wa majaji. Kesi ni nyingi,” alisema Othman. Hakuweza
kueleza mara moja idadi kamili ya majaji inayotakiwa ili kukidhi
mahitaji lakini akasema kuwa Serikali imeliona hilo na imekuwa
ikilifanyia kazi hatua kwa hatua.
Licha ya upungufu wa majaji,
Jaji Othman alisema wanakabiliwa na tatizo la kutumia teknolojia ya
zamani ya kusikiliza na kuandika tofauti na maendeleo ya sasa ambayo
yanahitaji kurekodi.
“Mfumo huu wa kutumia teknolojia ya kisasa pia
ungeweza kuharakisha kesi,” alisema Jaji Othman lakini akasema Kitengo
cha Biashara tayari kimeanza kuifanyia kazi teknolojia ya kisasa. Kwa
kutumia teknolojia hiyo, alisema mtu anaweza kutumia simu yake ya
mkononi kujua siku ya kesi yake na hata kuperuzi kwenye mtandao kupata
hukumu pamoja na mwenendo wa kesi yake.
Alisema wanatarajia kwenda
hatua kwa hatua ili kuhakikisha teknolojia hiyo ya kurahisisha kazi za
mahakama inaenea idara zote za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. Majaji
wengine wapya nao walisema kwenye mahojiano na waandishi wa habari
kwamba moja ya changamoto ni kufanya kazi katika mazingira magumu na
wingi wa kesi zilizolundikana katika mahakama hiyo.
Jaji Mutungi
alisema yeye anaamini kiu kubwa ya Watanzania ni kupatiwa haki na
kwamba haki hiyo inapocheleweshwa pia ni tatizo jingine. Ili
kuhakikisha anawatekelezea Watanzania haki zao, Mutungi alisema
atajitahidi kufanya kazi kwa bidii na kumaliza kesi nyingi kwa haraka.
Kwa upande wake, Jaji Mgeta alisema pamoja na wingi wa kesi kazi kubwa wanayopaswa kuifanya ni kuwa waadilifu na watenda haki. Alikiri
kwamba Tanzania wako nyuma katika teknolojia ya kuendesha kesi lakini
akasema hilo halipaswi kuwa ni jambo ambalo litawafanya warudi nyuma na
kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.
Chanzo: Mwananchi