Baada ya ukimya wa miezi kadhaa, Kiongozi wa Upinzani nchini
Uganda, Dokta Kiza Besigye amejipanga kuamsha upya ari ya wananchi wa
taifa hilo na kuingia mitaani, wakiandamana kuipinga serikali.
Wapinzani nchini Uganda wanapanga kurejea katika maandamano ya kuipinga
serikali mwezi huu, licha ya marufuku iliyoliwekea kundi la Activists
for Change yaani wanaharakati wa mageuzi, ambalo ndilo lililoanzisha
maandamano hayo bega kwa bega na kiongozi wa upinzani, Dokta Kiza
Besigye.Dokta Besigye anataka kutumia visa vya miaka mingi vya ufisadi, uvunjaji wa haki za binadamu na tuhuma za nyuma kuhusiana na wizi wa kura, mbinu inayolenga kuwatia shime wafuasi wake na kurejea mitaani kama ilivyotokea mwaka jana.
Mgombea huyo wa nafasi ya urais kwa mara tatu, anapania kutumia maandamano hayo kumpindua mpinzani wake wa siku nyingi, Rais Yoweri Museveni, ambaye Besigye anamtuhumu kwa kuiba kura.
Ni yapi hasa yanayowatatiza raia wa Uganda?
Ingawaje suala la gharama kubwa za maisha, zilichochea vuguvugu la ``walk to work´´ mwaka jana, kwa kiasi fulani halikufanikiwa katika kuhamasisha ghadhabu ya wananchi, wachambuzi wa mambo wanasema machungu ya huduma mbovu za umma, ufisadi uliokithiri na uvunjaji wa haki za binadamu miongoni mwa changamoto zingine, zinaweza kuamsha hisia kali kwa wafuasi wa upinzani na hatimaye kuandamana.
Huduma ya maji safi na salama haipatikani mahala kote nchini Uganda kama ilivyo hapa mjini Kisenyi.
Hatua kali za serikali dhidi ya waandamanaji mwaka jana zilisababisha
vifo vya watu wasiopungua tisa na Besigye, anayeongoza chama kikubwa
zaidi cha upinzani nchini Uganda, Forum for Democratic Change (FDC)
alimwagiwa pilipili machoni na kuwa nusu kipofu wakati fulani.Swali muhimu kwa sasa ni: Je! Besigye atafanikiwa kuwahamasisha wafuasi wake kuingia mitaani na kuipinga serikali baada ya unyamavu wa muda mrefu?
Na kwa upande wa mwitikio wa vyombo vya usalama: Iwapo polisi watatumia nguvu kubwa kuzimisha maandamano hayo, ni dhahiri itachochea ghadhabu ya umma na hofu kubwa juu ya usalama wa waandamanaji hao.
Sheria ya Kupinga Uhusiano wa Jinsia Moja
Muswada unaopendekeza adhabu kali dhidi ya watu wenye uhusiano wa jinsia moja umeletwa tena bungeni na David Bahati, mbunge kutoka chama tawala, National Resistance Movement, NRM.
Rasimu yake ya mwanzo ilipendekeza adhabu ya kifo kwa watu waliorudia kosa hilo, na baada ya kifungu hicho kupitiwa upya, rasimu mpya inatarajiwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa watu wanaorudia kosa hilo.
Jambo la kutiliwa maanani kwa sasa ni kuwa, iwapo muswada huo onevu utaridhiwa na bunge, hatua hiyo inaweza kuzishawishi nchi fadhili kupunguza misaada, ambayo ni robo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 ya serikali ya Uganda.
Yoweri Museveni, kiongozi aliyekaa madarakani kwa miaka mingi sasa.
Migogoro ya Mafuta na KodiKama vile haitoshi, mipango ya Uganda kuanza kuzalisha mafuta imeanza baada ya Kampuni ya Uingereza ya kuchimba mafuta Tullow, kuingia makubaliano mwezi Februari mwaka huu na Kampuni ya China, CNOOC, na Kampuni ya Total ya Ufaransa, ya kuendeleza vyanzo ya mafuta.
Pamoja na washirika hao wawili, Tullow inatarajia kutumia zaidi ya dola milioni 750 katika kutafuta na kuchimba mafuta mwaka huu pekee. Fedha hizo ni sehemu ya uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 10 ambapo makampuni hayo matatu yamezitenga kwa miaka michache ijayo, kwa ajili ya kujengea miundombinu kama vile kiwanda cha kusafishia mafuta ili kuanza biashara ya uzalishaji.
Wakati uzalishaji huo unaanza, migogoro na serikali juu ya masuala ya kisera inaanza kujitokeza, na matokeo yake ni kuchelewesha uzalishaji wa mafuta ghafi.
Na iwapo migogoro ya kodi haitatafutiwa ufumbuzi mapema, Uganda itaharibu sifa yake ya kuonekana kama si nchi sahihi inayostahili uwekezaji kutoka nje.
Kama uzalishaji ukianza mara moja, serikali itaweza kukabiliana na maandamano kwani itapata mapato kutokana na mafuta na hivyo kutumia fedha nyingi zaidi kuimarisha huduma za jamii.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\Reuters
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!