Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amelitaka Jeshi la Polisi
kuongeza weledi kwa kujifunza mbinu za kupambana na wahalifu wa kutumia
mitandao.
Dk Nchimbi alitoa kauli hiyo katika hotuba yake
iliyosomwa na Katibu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil wakati wa
uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Vyuo vya Polisi nchini, kuwa hivi sasa
watu wanatumia mitandao katika wizi ambao unaligharimu taifa.
Alisema
maofisa wa Jeshi la Polisi wanapaswa kujifunza na kujiimarisha katika
ujuzi wa mbinu wanazotumia wahalifu, ili kuwanyima nafasi ya kutenda
uhalifu.
“Matumizi ya mitandao yamevuka mipaka na kuanza kuwa
haramu na hivyo kuhitaji utaalamu wa hali ya juu kubaini uhalifu na
wahalifu,” alisema Abdulwakil na kuongeza:
Kuna kasi kubwa ya
matumizi ya fedha chafu, kuingiliwa kwa mifumo ya kibenki, mbinu za
kuhujumu mifumo ya kodi, matumizi ya teknolojia kukiuka sheria na
kutenda makosa mbalimbali ya jinai.
“Kwa mantiki hiyo mahitaji ya
kuwa na Jeshi la Polisi ambalo ni la kisasa, lenye weledi na ambalo
lipo karibu na wananchi hayakwepeki,” alisema Abdulwakil.
Kwa
upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema alisema kupitia
bodi hiyo itakayokuwa ikimshauri jinsi ya kuboresha vyuo vya jeshi hilo
ili kuwa na maofisa walioelimika na kukabiliana na uhalifu kwa ufanisi.
“Ukishakuwa
na askari aliyeelimika vizuri nina hakika hata uwajibikaji wake kazini
hususan kuwatumikia wananchi na Jeshi la Polisi, utakuwa wenye weledi
mkubwa,” alisema Mwema na kuongeza:
Askari anatakiwa kuhakikisha
anajua mapema tukio kabla ya kutokea, na hili litafanikiwa
tukiwashirikisha wananchi kwa ukaribu na hilo, ndilo litakiwa mafanikio
ya kupambana na wahalifu.
Bodi iliyozinduliwa ina wajumbe 18 kutoka
Tanzania bara na Zanzibar kutoka ndani na nje ya Jeshi la Polisi, chini
ya uenyekiti wa Profesa Florens Luoga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Luoga alisema wataitumia nafasi hiyo kumshauri IGP Mwema ili kulifanya jeshi hilo kuwajibika ipasavyo.
“Tunaelewa
changamoto zilizopo na tutahakikisha tunashirikiana ili kuziondoa na
kufikia malengo ya kuwa jeshi imara na lenye weledi,” alisema Profesa
Luoga.
SOURCE: MWANANCHI
July 4, 2012
NCHIMBI: POLISI KUTHIBITI WIZI MTANDAONI
Millionfortune.com
SIASA
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget