Mvutano huo ulitokana na klabu kutaka mchezo wao wa fainali uhamishiwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa madai ya kutoridhika na mazingira mabovu ya Uwanja wa Aman ambao umekuwa ukitumika kwa michuano hiyo.
Hii itakuwa mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo Visiwani, baada ya kupambana kwenye hatua ya makundi na kwenda sare ya bao 1-1.
Simba ilifanikiwa kusonga mbele hatua ya fainali baada ya kuifunga timu ya vijana ya Zanzibar (U23) bao 1-0, huku Azam nayo ikiitambia Superfalcon kwa mabao 3-2.
Simba chini ya Kocha Milovan Cirkovic ilikuwa na mastaa wake wote kwenye michuano hiyo akiwatumia kwa zamu kwa lengo kujua uwezo kila mmoja.
Kanu Mbiyavanga ndiye alifunika kwa wachezaji wapya na tegemeo kikosini hapo pamoja na Abdallah Juma, Mussa Mudde, Salum Kinje, Danny Mrwanda na Lino Masombo.
Akizungumza Mwananchi jana, Milovan ambaye anapenda kutumia mfumo wa 4-4-2 alisema: "Niko tayari kwa mchezo, ubingwa utakuja kwetu."
"Utakuwa mchezo mgumu, lakini nasi tumejiandaa kuona tunashinda kwa sababu nina wachezaji bora," alisema Milovan anayekisifu kikosi chake kwa kucheza soka la pasi.
Kocha Msaidizi wa Azam, Kali Ongala alisema: "Tumejiandaa vizuri na kwa sababu tutacheza Uwanja wa Taifa ambao hauna usumbufu wowote subirini soka ya uhakika."
"Mechi itakuwa ngumu kwa sababu Simba nao ni wazuri, lakini kikosi changu ni bora nakiamini watafanya vizuri na kuchukua Kombe hilo," alisisitiza Kali.
Azam inawategemea, Kipre Tchetche, Odhiambo na Gaudence Mwaikimba katika safu ya ushambuliaji.
Viungo ni Kipre Bolou, Ibrahim Mwaipopo, mabeki ni Said Murad, George Owino, Ibrahim Shikanda na Haji Nuhu.
Wakati huohuo, Kampuni ya Prime Time Promotions, wamepewa dhamana ya kuitangaza fainali hiyo itakayoanza saa 12 jioni.
Kiingilio cha juu kwenye mchezo huo kitakuwa Sh30,000 (VIP A), Sh20,000 (VIP B), 15,000 (VIP C), huku mashabiki watakaoketi jukwaa la rangi ya Chungwa wakilipa Sh10,000 na rangi ya Bluu na Kijani ni Sh5000.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!