Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina
Kombani amesema Serikali inatarajia kufanya tathmini ya utendaji na
majukumu ya kazi kwa watumishi wa kada za afya ikiwamo Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili.
Kombani alisema Tume ya Utumishi wa Umma
itafanya hivyo ili kupunguza mlundikano wa watu hasa wauguzi katika
eneo moja jambo ambalo linachochea kukiukwa kwa maadili.
“Kumekuwapo
na ongezeko la watumishi katika eneo moja, hili husababisha utendaji
mbovu na kukua kwa migogoro kwa hiyo tutafanya tathmini ya utendaji wa
watumishi hao na kujua majukumu yao kisha kupangua na kupunguza idadi
katika eneo moja,” alisema Kombani.
Kombani alisema hayo
alipokuwa akitoa majibu ya hotuba yake kwa wachangiaji ambapo awali,
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rosweeter Kasikila alihoji kuhusu wauguzi
kuwa na kurugenzi maalumu kutokana na wingi wao.
Aidha Kombani
alisema hoja ya kuwaongezea watumishi wa kada ya afya na elimu asilimia
50 ya posho kwa ajili ya mazingira magumu ya kazi, haitawezekana kwa
sababu kila kada inafanya kazi katika mazingira magumu kulingana na eneo
waliopo.
“Suala la asilimia 50 ya fedha kwa ajili ya mazingira
magumu ni la watu wote, hatuwezi kuzipa kada hizi mbili tu kwa sababu
hata kada nyingine nazo zinafanya kazi katika mazingira magumu,”
alisema.
Kombani alitoa mfano wa jinsi mbunge wa Nkasi Kaskazini
(CCM), Ally Keissy ambaye hutumia mitumbwi kufika katika maeneo ya
jimboni mwake na kusema kuwa, hayo ni baadhi ya mazingira magumu ya
kazi.
Alisema Serikali imeshafanya tathmini ya jinsi ya
kuwapunguzia adha ya mazingira magumu watumishi wake wa kada zote
ikiwamo kuwapa motisha.
July 5, 2012
WAFANYAKAZI MUHIMBILI KUPANGULIWA
Millionfortune.com
SIASA
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget