WANASAYANSI
wanaohudhuria Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi wameweka hadharani
baadhi ya tafiti ambazo zimetoa mwanga wa mapinduzi katika kupata dawa
za kinga, tiba na chanjo ya ugonjwa huo. Wanasayansi hao wamezitaja baadhi ya tafiti hizo kuwa ni HPTN 052 iliyowezesha upatikanaji wa dawa ya kuzuia maambukizo na ya pili, ni upandikizaji wa dawa kwenye mifupa, ambao ulionyesha kutibu Ukimwi. Tafiti ya tatu ni ile ya uwezekano wa chanjo, ambapo baadhi ya makundi maalumu ya watu wamegundulika kujijengea wenyewe kinga dhidi ya virusi. Wanasayansi hao walieleza hayo katika siku ya tatu ya mkutano huo unaofanyika Washington DC, Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni wao wakiwamo wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo toka karibu kila kona ya dunia. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Mkutano huo na gazeti hili kupata nakala yake, wanasayansi hao walisema dawa za kuzuia maambukizo ni moja ya silaha kubwa kuelekea kupata ushindi dhidi ya kupiga vita Virusi Vya Ukimwi (VVU). Walitoa mfano wa utafiti uliopewa jina HPTN 052 ambao umeonyesha kuwa, unawezesha kupunguza maambukizo ya VVU kwa asilimia 96. Katika utafiti huo, dawa hiyo imeonekana kufanya kazi vizuri zaidi pale mwathirika anapotumia dawa hiyo mapema wakati seli nyeupe za kinga aina ya CD4 zikiwa kati ya 350 na 550 kwa kila milimita za ujazo za damu. “Tiba kwa ajili ya kuzuia maambukizi ni sayansi ambayo imechangia mapinduzi makubwa katika kukabili VVU tangu dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV) zianze kutumika duniani mwaka 1996,” alisema Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira na kuongeza kuwa, “ARV zimeweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani. Dk Katabira aliongeza: “Mpango mzuri uliohamasishwa na wanasayansi katika matumizi ya ARV, hasa katika nchi zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo, umewezesha matokeo chanya ya mkakati wa kukabiliana na Ukimwi.” Kuhusu upatikanaji wa tiba ya Ukimwi, wanasayansi hao walizindua mpango kabambe wa dunia wa namna ya upatikanaji wa tiba. Naye Makamu Mwenyekiti wa mkutano huo, Dk Diane Havlir akasema: “Huu ni mkutano ambao wanasayansi wamethibitisha kuwa tiba ya Ukimwi ipo karibu kupatikana.” Naye Dk Havlir ambaye pia ni Mtaalamu wa Tiba katika Chuo Kikuu cha Calfornia, Marekani aliongeza: “Matumaini ya wanasayansi kwenye mkutano wa mwaka huu kwamba upatikanaji wa tiba yanaashiria hatua iliyopigwa na wataalamu hao katika miaka michache ya karibuni.” Dk Havlir alifafanua; “Ndiyo maana tunazungumzia kuhusu ufumbuzi wa kisayansi wa kutatua tatizo hili, ambao hatukuthubutu kuutamka miaka kadhaa iliyopita,” Dk Havlir alieleza kuwa, matokeo kadhaa ya tafiti hizo za kisayansi yameleta mapambazuko mapya katika kupata tiba. Dk Havlir aliuzungumzia utafiti ambao alifanyiwa mwathirika wa VVU wa Ujerumani, Timothy Brown ambaye dawa iliyopandikizwa kitaalamu na wanasayansi kwenye mifupa yake ilimwezesha kumponya kabisa na hana tena VVU. Utafiti wa Tanzania Wataalamu hao pia walizungumzia utafiti ambao pia madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, Tanzania walichangia kwa kiwango kikubwa katika kuufanikisha. Dk Havlir aliuelezea utafiti huo kuwa ni ule uliobaini kuwa, kuna baadhi ya watu ambao baada ya kuambukizwa VVU walijijengea kinga madhubuti na wameendelea kuishi pasipo matatizo. Gazeti la Mwananchi toleo la Desemba 2, mwaka jana liliripoti juu ya utafiti huo ambapo wanasayansi wa Tanzania walishiriki katika kuufanikisha. Kiongozi wa ushirikiano wa kitafiti kati ya KCMC na Chuo Kikuu cha Afya cha Duke nchini Marekani, Dk Elizabeth Reddy alinukuliwa akisema; “KCMC ilisaidia sana kufanikisha utafiti huo ambao utawawezesha wanasayansi kupata chanjo.” Katika siku hiyo ya tatu ya mkutano huo ulioanza Jumapili wiki iliyopita, wanasayansi kadhaa walitoa hoja zao kuhusu mapambano ya Ukimwi na kuhimiza juhudi za kisayansi za kupata tiba kamili. Katibu Msaidizi wa Idara ya Afya Marekani, Dk Howard Koh alisema nchi yake ina mpango kabambe wa kitaifa kuokoa maisha ya waathirika kwa ushirikiano na mataifa mengine duniani. Mtaalamu kutoa Taasisi ya Utafiti wa Ukimwi ya IrsiCaixa, Javier Martinez-Picado alisisitiza kuwa ajenda ya upatikanaji wa tiba ya ugonjwa huo ndiyo mbinu madhubuti zaidi inayopaswa kufanikishwa na wanasayansi. Mtaalamu wa utafiti wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta iliyopo Nairobi nchini Kenya, Dk Nelly Mugo alizungumzia juu ya umuhimu wa matumizi ya dawa za ARV kuzuia maambukizo kwa watoto wakati wa kujifungua. Alisema mpango huo umesaidia kwa kuokoa maisha ya watoto wengi waliozaliwa kuambukizwa VVU. Katika siku ya pili ya mkutano huo, watafiti hao waliweka bayana kuwa VVU siyo tishio tena kwa dunia kwa sababu wanazo nyenzo zote za kukabiliana nao ila kinachotatiza ni fedha. Walisema fedha zitawaongezea nguvu katika kufanikisha mipango ya kisayansi pamoja na uwekaji wa sera zitakazosaidia mapambano thabiti dhidi ya VVU. |
July 27, 2012
Wanasayansi wataja kinga, tiba za Ukimwi
Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!