THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA MINISTRY OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM
TAARIFA KWA UMMA
HAKUNA MPANGO WA KUWAHAMISHA WAMASAI
Wizara ya Maliasili na Utalii inasisitiza kuwa hakuna mpango wowote wa kuwahamisha Wamasai 48,000 kutoka Serengeti, wala popote pale nchini, ili kupisha shughuli za uwindaji.
Hii ni taarifa ya pili kutolewa na Wizara kukanusha kampeni ambayo inaendelea kusambazwa kupitia mtandao wa kompyuta wa Avaaz inayowataka watu wajiorodheshe kupinga kuhamishwa kwa Wamasai kutoka Serengeti.
Hata hivyo mtandao huo umeendelea kusambaza habari hizo na kuwataka watu wajiorodheshe ili kupinga mpango huo na kuiandikia Wizara wakiitaka iusitishe. Hata hivyo sasa wamebadilisha tamko lao na kusema kuwa walipotaja Serengeti katika taarifa yao ya awali walimaanisha kuwa ni eneo lote lililoko kwenye Mfumo ikolojia wa Serengeti (Serengeti ecosystem). Hali hii inafuatia Taarifa ya kwanza iliyotolewa Agosti 15, mwaka huu ambapo Wizara ilikanusha kuwepo kwa mpango huo.
Wizara imewataka watu na Jumuiya ya kimataifa kutopoteza muda wao kujiorodhesha kupinga kuhamishwa kwa Wamasai maana wamepotoshwa kwa kuwa hakuna mpango kama huo popote pale nchini Tanzania. Uwindaji wa kitalii hufanyika katika Mapori ya Akiba na siyo katika maeneo wanayoishi wananchi, hivyo shughuli hiyo haiambatani na kuhamishwa watu.
Watu wote ambao wamejiorodhesha baada ya kupotoshwa na mtandao huo wanaalikwa kuja nchini kama watalii ili waitumie fursa hiyo kujionea wenyewe taratibu za uhifadhi zilivyo nchini na kujidhirisha kuwa taarifa iliyotolewa na mtandao huo siyo ya kweli.
Imetolewa na
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 24 Agosti 2012
Simu: +255 784 468047
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!