Kufuatia mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, waandishi wa habari nchini wamepanga kufanya maandamano ya amani kesho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam, katika kikao kilichoandaliwa na TEF, chini ya Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Nchini (TEF), Theophil Makunga.
Aidha, madhumuni makubwa ya kufanya maandamano hayo ya amani ni kueleza huzuni iliyowapata wadau na tasnia ya habari hapa nchini kufuatia mauaji ya Mwangosi, kwani tangu kupatikana kwa uhuru wa taifa hakuwajawahi kutokea kwa tukio la kusitikisha kama hilo katika tasnia hiyo.
Kwa mujibu wa TEF, jijini Dar es Salaam maandamano hayo yatafanyika kesho kuanzia saa 2:00 asubuhi, ambapo yataanzia ofisi za Channel Ten, kupitia mitaa ya Azikiwe hadi Barabara ya Bibi Titi, na kuhitimishwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako mkutano utafanyika.
Maandamano hayo yameratibiwa na vyama vya habari (press clubs) kote nchini na kuhusisha wadau wote wa tasnia ya habiri ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari.
Mwangosi alifariki dunia Jumapili wiki iliyopita katika Kijiji cha Nyololo Mufindi, mkoani Iringa na kuzikwa jijini Mbeya, wiki hiyo hiyo, baada ya kuuawa kwa kupigwa na kitu mithili ya bomu lililopelekea mwili wake kusambaa vipande vipande.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!