JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
KUUWAWA KWA JANGILI KATIKA PORI LA AKIBA BURIGI
Usiku
wa tarehe 13 (kuamkia tarehe 14) Agosti 2012 mtu mmoja jangili ambaye
jina halijapatikana aliuwawa katika Pori la Akiba la Burigi Mkoani
Kagera baada ya mapambano kati ya genge la majangili na askari wa
Wanyamapori waliokuwa wakifanya doria ndani ya pori hilo.
Siku hiyo mnamo saa 7 usiku askari wanyamapori walisikia milio ya risasi katika eneo la Nyungwe Kilomita 5 ndani ya Pori la Burigi. Askari walifika katika eneo la tukio maana walikuwa wakifanya doria karibu na eneo hilo na kukuta majangili ambao walikuwa wamemulika tochi zenye mwanga mkali.
Majangili
walianza kurusha risasi walipobaini kuwa askari wamewakaribia. Askari
Wanyamapori walijibu mapigo na mapigano hayo yaliendelea kwa muda wa
takriban saa moja kabla ya majangili kukimbia.
Ilipofika
saa moja asubuhi, wakati walipokuwa wanakagua eneo la tukio, askari wa
Wanyamapori waligundua kuwepo kwa maiti akiwa na bunduki aina ya gobore
na baruti. Askari Wanyamapori walitoa taarifa katika kituo cha Polisi
Biharamulo ambapo Polisi waliuchukua mwili wa Marehemu na kuupeleka
katika hospitali ya Biharamulo ambako mwili umehifadhiwa hadi sasa.
Hadi
leo hakuna mtu aliyejitokeza kudai kupotelewa na ndugu. Hata hivyo
uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 20 hadi 28 anaweza akawa ni raia wa nchi jirani.
Uchunguzi unaendelea.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NAUTALII
16th Agosti 2012
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!