MBIO za kuwania nafasi za uongozi wa juu wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi (CCM), imeshika kasi huku taarifa zikionyesha kwamba kambi zinazowania urais wa 2015 ndani ya chama hicho, kila moja inajipanga kuhakikisha inaweka watu wake. Wakati katika Umoja wa Wanawake (UWT) hadi jana mchuano ulikuwa ukionyesha kuwa mkali kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela hali ni tofauti kwa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM). Hadi jana katika mbio za kuwania nafasi ndani ya UVCCM, vijana wanne walikuwa wamechukua fomu kuwania nafasi ya uenyekiti na wengine 16 wakiomba nafasi ya makamu mwenyekiti wa jumuiya hiyo ngazi ya taifa huku Katibu Mkuu wa Umoja huo, Martine Shigella akisema wanafahamu mikakati hiyo ya kambi za urais. Kwa upande wa UWT, Kilango anaonekana kusimama kundi la makada wa CCM wanaojipambanua kupambana na ufisadi, huku Simba akiwa na kundi jingine tofauti na hilo lakini, pia lenye malengo ya urais wa 2015. Baadhi ya vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM, vilisema mbali ya nafasi hiyo ya juu ya UWT, kinyang’anyiro hicho pia kipo katika nafasi za wenyeviti wa mikoa. Tayari vita hiyo ya kambi za urais iko pia katika mikoa ambako kila kambi inajipanga kuweka mtu wake, huku katika Mkoa wa Tabora vita ikitarajiwa kuwa kali zaidi kati ya Margareth Sitta na mgombea wa kambi ya watuhumiwa wa ufisadi. UVCCM Kwa upande wa umoja huo wa vijana, kambi hizo zimekuwa zikiumana kuhakikisha kila moja inaweka mtu wake katika nafasi ya uenyekiti, makamu na ujumbe wa Baraza Kuu. Hadi jana waliokuwa wakiwania nafasi za uenyekiti wa UVCCM Taifa ambao tayari walikuwa wamerejesha fomu ni Thabit Jecha Kombo, Sadifa Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka. Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Paul Makonda, Ally Salum Hapi na Agustino Matefu. Makonda alirejesha jana na kuzungumza na waandishi akiahidi kupambana na mafisadi. Wanaowania nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec), kupitia UVCCM ni Theresia Mtewele, Halima Bulembo, Olivia Sanare, Ahmed Nyangani, Santo Tena, Vaileth Sambilwa, Faidha Salim na Augustino Samwiya. Katika nafasi za Ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa ni, David Mwakiposa, Mteweke Bulembo na Ester Mambali. UVCCM ni ngome muhimu kimkakati kutokana na kuwa na vijana wengi wanaoweza kufanikisha ajenda mbalimbali ndani na nje ya vikao vya chama na jumuiya. Uchaguzi huo wa UVCCM unafanyika wakati, kiti cha mwenyekiti kikiwa wazi tangu mwaka 2010 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Yusuf Hamad Masauni kuong’olewa akituhumiwa kudanganya umri na tangu wakati huo nafasi yake ilikuwa ikishikiliwa na Makamu wake, Beno Malisa. Taarifa ya Sekretarieti ya chama hicho iliyowasilishwa katika kikao cha NEC mjini Dodoma mapema mwaka huu ilieleza kuwa makundi ya urais 2015 ndiyo yanayosababisha mpasuko ndani ya chama hicho. Shigella: Tunajua Akizungumzia mikakati hiyo ya vigogo wanaotaka urais kumwaga fedha ili kujiweka mazingira mazuri ya kuwa na watu wao ndani ya UVCCM, Shigella alisema wanajua mipango hiyo na kuonya kwamba kama kuna mgombea ambaye ametumwa na genge la watu wanaotarajia kuwania urais 2015, ajue anapoteza muda kwa sababu hatapitishwa. Alisema jumuiya hiyo haijawahi kuwa na kiongozi aliyepandikizwa na mtu yoyote. Alisema watatumia njia mbalimbali kuwabaini watu wa aina hiyo, hasa kwa kuitumia Kamati ya Usalama na Maadili ya jumuiya hiyo na kuwafanyia usaili wagombea na kuangalia historia zao. “Kwa hiyo, kama kuna wanaowania nafasi za urais mwaka 2015 ambao wametuma vijana kutafuta nafasi UVCCM wafahamu kuwa hawatafanikiwa kwa kuwa tumejiandaa kukabiliana nao,” alisema Shigela. Makonda na ufisadi Kwa upande wake Makonda ambaye jana alikuwa wa mwisho kurejesha fomu kwa wiki iliyoisha jana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa tatizo la rushwa na ufisadi kwa baadhi ya watu ndani ya UVCCM ndilo lililomsukuma kuwania nafasi hiyo. Alisema historia ya UVCCM kutoka Tanu Youth League imejengeka katika misingi ya uadilifu na uzalendo, lakini katika siku za karibuni kumekuwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi ambao wamekuwa wakibomoa misingi hiyo na kujenga ya kwao ya kifisadi. “Hii ndiyo changamoto ambayo imenifanya nijitose katika kinyanganyiro hiki, si vizuri kuhama chama kikiwa na matatizo. Njia sahihi ni kutafuta uongozi ili kukabiliana nayo. Tukiwa na viongozi bora tutakuwa na uchungu wa namna ya kutatua matatizo ya vijana, kama uchumi na hata mikakati ya ajira,” alisema. Alisema wakati rushwa ilitajwa kama adui wa haki katika moja ya ahadi 10 za Mwana-TANU, sasa hivi imekuwa ikitumika kama haki ya kupata uongozi hivyo vijana wanyonge wasiokuwa na fedha za kutoa rushwa kukosa nafasi za kuongoza. Nape: Tumejipanga Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema hafahamu kama kuna vijana wanaowania nafasi mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia vigogo kwenye mbio za urais mwaka 2015. “Ndiyo kwanza unaniambia, sina habari hizo. Katika CCM tunachoangalia ni kwamba wanaowania nafasi hizo ni kutojihusisha na rushwa vinginevyo hawatakuwa na sifa za kuchaguliwa,” alisema Nape. Source: http://www.mwananchi.co.tz/ |
August 7, 2012
Urais 2015 wavuruga chaguzi za CCM
Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!