TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI ALIUNDA KAMATI SIO TUME
Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi inapenda kutoa taarifa kwa Umma kuwa katika kikao chake na Waandishi wa Habari cha tarehe 4 Septemba, 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alitoa taarifa ya kuunda Kamati kuhusiana na vurugu zilizotokea katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, tarehe 2 Septemba, 2012 ambapo katika vurugu hizo mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi alipoteza maisha.
Waziri Nchimbi alisema aliunda Kamati hiyo, (na siyo Tume), ili kumsaidia kupata majibu ya maswali yafuatayo, ambayo alisema hakuwa na majibu yake:
1. Nini kilikuwa chanzo cha kifo cha mwandishi wa habari, Bw. Daudi Mwangosi,
2. Kama upo uhasama kati ya waandishi wa habari wa Iringa na Polisi,
3. Kama ipo orodha ya waandishi watatu (3) waliopangwa kushughulikiwa na Polisi,
4. Kama ukubwa wa nguvu za Polisi zilizotumika ulikuwa sahihi,
5. Kama zipo taratibu zinazoruhusu Vyama vya Siasa kukata rufaa visiporidhika na maamuzi ya Polisi,
6. Kama kuna tatizo la mahusiano kati ya Polisi na Vyama vya Siasa.
Taarifa hii inatolewa ili kuweka sawa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vikimnukuu Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tindu Lissu akisema Chama chake hakiungi mkono Tume ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha televisheni cha Channel Ten, kwa madai kwamba imeundwa kinyume cha Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 1962 Sura ya 29, ambayo alisema kwa mujibu wa Sheria hiyo, tume zote za uchunguzi huundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupitia taarifa hii, tunapenda kuuarifu Umma kuwa Waziri Nchimbi hakuunda Tume ila aliunda Kamati hiyo kwa Mamlaka aliyonayo kama Waziri na uundaji wa Kamati hii hauhusiani kwa vyovyote na matakwa ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, Marejeo ya Mwaka 2002.
Utaratibu wa kutumia Kamati kutafiti jambo kwa kina kwa ajili ya kumshauri Waziri au kiongozi mwingine yoyote ni wa kawaida katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya umma.
Imetolewa na Isaac J. Nantanga
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
06 Sepemba, 2012
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!