Taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA) imezindua mfuko wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 7.5 kufadhili miradi ya ubunifu katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayolenga kuondoa vikwazo vya biashara katika kanda hiyo.
TMEA ni taasisi inayofadhiliwa na mashirika mbalimbali ili kuunga mkono juhudi za kusukuma mbele masuala ya mtangamano hususan ni katika biashara na uchumi katika kuimarisha mkataba wa mtangamano wa EAC.
Mradi huo unaojulikana kama ‘’Mfuko wa Changamoto wa Taasisi ya Trade Mark East Africa ‘’ uliziduliwa rasmi katikati mjini Kigali, Rwanda na Mkurugenzi wa Afrika Mashariki wa taasisi hiyo, Mark Priestly.
Mfuko huo utakaoendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu unalenga sekta binafsi na vyama vya kiraia, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.
Priestly alibainisha kuwa changamoto kama vile kuwepo kwa vikwazo visivyo vya ushuru na mchanganyiko wa vuzuizi vya usambazaji, ni masuala ambayo bado yanazuia mtiririko mzuri wa uendeshaji wa biashara katika kanda.
“Sisi hasa tunatafuta ubunifu na mawazo mapya ya kuchangamsha biashara katika Jumuiya EAC na kukabiliana na changamoto ambazo inakumbana nazo,” aliongezea.
Uwekezaji mkubwa katika ubunifu wa miradi ulianza na sekta binafsi na vyama vya kiraia ambavyo vinaweza kukuza biashara katika kanda ndani ya EAC.
Mfuko huo umeshaanzishwa nchini Kenya na Tanzania na muda si mrefu utazinduliwa pia katika nchi za Burundi na Uganda.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Rwanda, Francois Kanimba, alisema mfuko huo ni mpango mwafaka ambao utakuza juhudi za nchi yake kubadilisha uchumi na kuwa mhimili wa kutoa huduma kupitia usafirishaji bidhaa kwa wingi nje ya nchi.
Alisema Mfuko huo unatoa nafasi kwa Wanyarwanda kushindana kikanda kwa kuutumia ili kuendeleza biashara zao.
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!