Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
ASEMA FIGO ZAKE ZIMESHINDWA KAZI, ZATAKIWA DOLA 40,000 KUMPELEKA INDIA
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
imebadilika na kuwa mbaya, baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi ya
kuchuja sumu ya mwili na kusababisha apatiwe huduma ya kusafisha damu
yake.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi wa
jopo la madaktari wanaoendelea kumtibu, Profesa Joseph Kahamba,
zilieleza kuwa hali ya Dk Ulimboka ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo
kuwapo mikakati wa madaktari wenzake kukusanya fedha ili kumpeleka nje
ya nchi.
Dk Ulimboka ambaye amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa
Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI),
alipatiwa huduma hiyo jana asubuhi kwa kutumia mashine maalumu, iliyoko
katika Kitengo cha Watoto cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Daktari
huyo ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima
kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, amelazwa
kutokana na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili,
baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha,
meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia
Jumatano.
Tangu alazwe MOI baada ya kuokotwa na wasamalia wema,
katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dares Salaam, hali ya
afya ya Dk Ulimboka imekuwa tete na jana ilizidi kuwa mbaya.
Kauli ya Dk Kahamba
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Kahamba alisema kutokana na tatizo hilo, mgonjwa huyo jana alilazimika kusafishwa damu.
Alieleza
hayo alipotakiwa kuthibitisha taarifa zilizolifikia gazeti hili kuwa
afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri na madaktari wanachangishana fedha
kumpeleka kwenye matatibu ya kusafishwa damu katika Hospitali ya Regency
jijini Dar es Salaam au nje ya nchi.
"Taarifa hizo zina ukweli,
lakini siyo jambo rahisi kiasi hicho kwamba anatakiwa kusafishwa damu.
Kama ni damu amesafishwa leo (jana) asubuhi katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili," alisema Profesa Kahamba na kuendelea:
"Suala lake ni complicated (tata) zaidi, lakini ili watu waelewe, siyo mbaya mkisema figo zimefeli(zimeshindwa kufanya kazi)."
Alipotakiwa
kueleza sababu ya tatizo hilo, Profesa Kahamba alisema, "Siwezi kueleza
kwa undani ila haya maumivu ya kupigwa na kuteswa yanachangia kwa kiasi
kikubwa."
Alipotakiwa kueleza yeye anaonaje hali ya sasa ya Dk Ulimboka, Profesa Kahamba alisema: “Ni uongo tukisema anaendelea vizuri."
Aliendelea,
"Unajua alipofikishwa hapa Muhimbili juzi (Jumatano) afya yake ilikuwa
mbaya, na jana (Alhamisi) alionekana kuendelea vizuri, lakini jana
hiyohiyo, hali yake ilianza kubadilika na vipimo vilionyesha kuwa ana
complications (matatizo) za figo.
"Sasa figo ni kitu sensitive
(muhimu) sana, anahitaji uangalizi wa karibu na kimsingi hatuwezi kusema
kwamba anaendelea vizuri. Ni vyema tukisema tu afya yake ni mbaya,"
alieleza.
Taarifa za awali kutoka kwenye chanzo chetu hospitalini
hapo, zilieleza kuwa Dk Ulimboka ambaye alipata tatizo linalojulikana
kama “Acute renal failure”, alifanyiwa tiba inayojulikana kama Dialysis,
ambayo ni kitendo kutumia mashine maalumu kufanya kazi ya kuchuja sumu
ya mwili kwenda kwenye mkojo, baada ya figo ambazo hufanya kazi hiyo
kushindwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Dialysis inaweza kumsadia
mgonjwa ambaye figo zake zimeshindwa kufanya kazi, kuishi kama kawaida,
lakini kwa Dk Ulimboka haikutoa matokeo mazuri.
Michango ya madaktari
Jana
ulifanyika Mkutano wa Madaktari Bingwa wa MNH, Chuo Kikuu Sayansi ya
Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ocean Road (ORCI) na kuazimia kukusanya Dola
za Marekani 40,000 (Sh64,000,000) ili Dk Ulimboka asafirishwe kwenda
India kwa matibabu zaidi.
Taarifa za maazimio hayo zilitangazwa
kwa waandishi wa habari na Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin
Chitega, kuwa afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri hivyo zikipatikana fedha
hizo angepelekwa nje ya nchi.
Dk Chitega aliwataka wanataaluma
hao na wananchi kwa ujumla kuchangia safari hiyo ili kuokoa maisha ya
daktari huyo, huku akitaja namba za mawakala wa simu za Vodacom na Tigo,
ambazo zitatumika kukusanya michango hiyo.
Habari zilizopatikana
baadaye wakati tunakwenda mitamboni zilieleza kuwa, Dk Ulimboka
alitarajiwa kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.
TANNA MOI watoa tamko
Katika
hatua nyingine, Chama cha Wauguzi (Tanna), Tawi la MOI kilitoa tamko la
kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka na
kutaka uchunguzi wa kina na haraka ufanyike ili kubaini watu
waliohusika.
Mwenyekiti wa Tanna, Tawi la Moi, Prisca Tarimo
alisema katika tamko hilo kuwa, kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha
kinyama na kisicho cha kiutu.
Katika tamko hilo, Tanna imeomba
Serikali kutafuta suluhu ya mgomo huo haraka kwa kuwa unaathiri maisha
ya watu na kuwaongezea mzigo wa kiutendaji wauguzi.
Mgomo wa madakati unaingia siku ya saba leo, huku suluhu ya kuaminika ya kutatua tatizo hilo, ikiwa bado haijapatikana.
Polisi wakanusha
Katika
hatua nyingine, James Magai anaripoti kuwa, Jeshi la Polisi limekanusha
kumteka na kumjeruhi Dk Ulimboka, huku likipinga pia taarifa za daktari
huyo kumtambua mmoja wa askari walio katika jopo la uchunguzi wa tukilo
hilo alipokwenda kumtembelea hospitalini.
Pia jeshi hilo limetoa
wito kwa madaktari hao walioko katika mgomo kuwa na busara na kutii
amri ya Mahakama, ya kuwataka wasitishe mgomo wao.
Pia limeonya
kuwa ikiwa wataendelea kukaidi na kupuuza amri ya hiyo ya mahakama,
linao wajibu wa kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani, ili
wajibu mashtaka hayo.
Msimamo huo ulitolewa jana na Kamishna wa
Oparesheni Maalumu, Kamishna wa Polisi (CP), Paul Chagonja wakati
akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano alioitisha
kuzungumzia matokeo ya operesheni ya jeshi hilo ya majuma matatu katika
kuzuia uhalifu nchini.
Alisema madai hayo ni uvumi ambao unalenga
kulifanya jeshi hilo lisiaminike na kufifisha juhudi zake za kuwasaka
waliohusika na unyama huo.
Source: Mwananchi