Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
AELEZA MGODI ULIVYOUZWA BEI YA KUTUPA,NGELEJA NAYE AZUA MTAFARUKU BUNGENI
SAKATA
la ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani
Mbeya limeibuka upya, safari hii ikielezwa na Mbunge wa Musoma Vijijini
(CCM), Nimrod Mkono kuwa umeuzwa kwa bei ya kutupa.Mbunge huyo ambaye ni
mwanasheria, amelitaka Bunge kuunda Kamati Teule kwenda kuchunguza
ufisadi huo, huku akihoji sababu za Serikali kuutengea mabilioni ya
shilingi wakati umekwishauzwa.
Mkono alisema kuwa, “Mgodi huo
wenye thamani ya matrilioni ya shilingi, umeuzwa kwa bei ya kutupa ya
dola 700,000 tu za Marekani (Sh1.1 bilioni), kwa kampuni ya Intra Energy
ya Australia.”
Mgodi wa Kiwira uliwahi kuzua malalamiko baada
ya kumilikishwa kwa Kampuni ya ANBEN Limited, mali ya Rais Mstaafu
Benjamin Mkapa na mkewe, Anna Mkapa, lakini Januari mwaka huu, aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliieleza Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kuwa ANBEN Limited haihusiki tena
na mgodi huo.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo iliondolewa kuwa
miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa 200,000
ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa Kampuni ya Tan-Power Resources
(TPR).
Akichangia mjadala wa Bajeti jana, Mkono alihoji sababu za
Serikali kutenga Sh40 bilioni kwa ajili ya kulipa watu wa mgodi wa
Kiwira ilhali inajua kuwa mgodi huo uliuzwa kwa bei ya kutupwa tangu
mwaka 2007.
“Tumetenga Sh40 bilioni za kuwalipa watu waliotuibia
fedha zetu, eti tunasema kwamba tunalipa madeni, haya ni madeni gani
ambayo tunakwenda kulipa huko?” alihoji Mkono.
Alisema mwaka 2007
wabunge walipiga kelele wakiitaka Kampuni ya Tan Power iliyokuwa mbia
wa Serikali katika mgodi huo, kuurudisha serikalini, lakini mwaka jana
kampuni hiyo iliuza mgodi huo kwa bei ya kutupa.
“Unauzaje mgodi
huu wenye thamani ya matrilioni ya pesa kwa bei hii ya kutupa?” alihoji
na kuendelea, "Haya ni mambo ya ajabu sana. Tungeweza kupata fedha
nyingi sana kutokana na mgodi huu na fedha hizi zingetusadia katika
kugharimia mahitaji yetu ya bajeti.”
Mbunge huyo aliungana na
wabunge wengine kuiponda Bajeti ya Serikali kwa kutegemea fedha za
wahisani, huku rasilimali za nchi zikiendelea kufujwa bila huruma.
Alisema
nakisi inayoonekana kwenye Bajeti, inatokana na uwezo mdogo wa
kukusanya fedha za ndani licha ya kwamba nchi ina utajiri mkubwa wa
madini, ambayo hata hivyo, yanawanufaisha watu wengine na kuwaacha
Watanzania wakitaabika.
Mkono pia aliishambulia Serikali kwamba
‘ilichakachua’ mradi wa uchimbaji wa madini katika mgodi wa Buhemba na
kuwadanganya wananchi ambao hawakunufaika na kitu chochote.
Kutokana
na hilo, mbunge huyo alisema kuwa Bajeti ya mwaka 2012/13 imetoa
upendeleo kwa baadhi ya maeneo huku ikiyaacha mengine muhimu, ambayo
yanagusa masilahi ya wananchi.
“Serikali ilichakachua Buhemba
lakini inapeleka tena Sh1 bilioni huko na sijui zinakwenda kufanya nini
wakati ingeweza kupeleka katika moja ya shule za jimboni kwangu, au hata
kama ingetusaidia wananchi wa Mara kujenga chuo kikuu cha kilimo
ambacho kinajengwa mkoani kwetu,’’alisema Mkono.
Alisema yeye
binafsi haelewi Serikali inaposema haina fedha kwani migodi ya Kiwira na
Buhemba ingetumika vizuri, ingeweza kuipatia Serikali kiasi kikubwa cha
fedha kinacholingana na fedha zinazotolewa na wafadhili.
Ngeleja achafua hewa
Katika
hatua nyingine, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja jana
alisababisha mvutano mkubwa ndani ya Bunge na kuondoa utulivu kwa muda,
kutokana na mchango wake wa kuiponda Bajeti ya Upinzani.
Ngeleja
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi Mei 4, mwaka huu
alipong’olewa na Rais Jakaya Kikwete, aliwabeza wapinzani kuwa Bajeti
yao ilikuwa imeandaliwa na watu ambao wana maono ya kuandaa bajeti za
harusi na maandamano, lakini si katika hali ya kuandaa Bajeti ya nchi
kama Tanzania.
“Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu walio mbele yangu
hawana jipya, na ningependekeza wasimame na kuwaomba radhi Watanzania
maana wameandaa bajeti ya maandamano na harusi,’’ alisema Ngeleja.
Alisema Bajeti ya Upinzani ni ya ovyo na haikuainisha vyanzo mbadala vya mapato na hivyo kuwataka Watanzania kuipuuza.
Huku
akishangiliwa na mawaziri na wabunge na CCM, alisema kama viongozi wa
upinzani wanaitakia mema Tanzania, ni vyema wakatumia nafasi zao ndani
ya Bunge kusimama na kuwaomba radhi wananchi kwa kuwa wamesababisha
baadhi kutoijali mipango mizuri ya Serikali.
Hali hiyo ilisababisha wabunge wengi wa Chadema kusimama na kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu jambo hilo.
Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee walipewa nafasi ya
kuzungumza, huku Ngeleja akipinga kila kitu walichosema.
Mdee
alimweleza Spika kuwa tatizo la Ngeleja siyo kupingana na maoni ya Kambi
ya Upinzani bali ni hasira za kuondolewa katika nafasi ya uwaziri wa
Nishati na Madini, jambo ambalo bado linamuuma.
“Mheshimiwa
Spika, hakuna kitu kama hicho, tatizo la Ngeleja ni kuondolewa katika
nafasi ya uwaziri na siyo kitu kingine, maana kama ni maneno ambayo
yalikuwa yamekosewa tayari tulishaleta mabadiliko yake humu ndani,”
alisema Mdee, kisha akakubaliana na Spika, kuondoa maneno kuwa tatizo la
Ngeleja ni uwaziri.
Kwa upande wake Mbowe, alisema kuwa Ngeleja
hakusoma bajeti yao vizuri na kumwomba Spika kutoa tamko la namna ya
kuwashughulikia wote wanaodanganya umma katika michango yao.
Lissu
alitoa ufafanuzi ulioafikiwa na Spika, kuwa Bajeti inayojadiliwa
bungeni ni moja ambayo ni ya Serikali, na kwamba Kambi ya Upinzani haina
ya kwake, bali inatoa maoni kwa ile ya Serikali.
Chanzo cha habari: Mwananchi