Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe amefanya ziara ya kushtukiza
katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu Manispaa ya Morogoro na kufanya
ukaguzi wa mabasi ya abiria ambapo mabasi matatu aliyaamrisha yalipe
faini ya Sh250,000 kila moja kutokana na makosa mbalimbali likiwamo la
kutokuwa na dereva wa akiba.
Ziara hiyo aliifanya mapema wiki
hii asubuhi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambapo lengo la waziri
huyolilikuwa kukagua mabasi yanayofanya safari za mikoani na nje ya nchi
na kuona kama yanakidhi vigezo vya Sumatra katika shughuli ya
kusafirisha abiria.
Katika ziara hiyo, Dk Mwakyembe alifika
katika kituo hicho cha mabasi na kuegesha gari mbali kidogo kisha
kuelekea kwenye mabasi huku akijifanya abiria na kuingia ndani ya mabasi
hayo kisha kuanza kukagua leseni za madereva na vitambulisho vya
kampuni za mabasi wanavyotumia madereva.
Ukaguzi mwingine
alioufanya ni ratiba za safari pamoja na usalama wa mabasi na baadaye Dk
Mwakyembe aliamrisha madereva walioonekana kuwa na makosa kulipa faini
Sumatra.
Mabasi yaliyolipishwa faini ni pamoja na Royal Coach
linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba ambalo
dereva wake hakuwa na kitambulisho cha kampuni, basi la Super Najimunisa
na Muro Investiment yanayofanya safari zake Dar es Salaam kuelekea
Mwanza ambapo mabasi hayo yalikuwa na kosa la kutokuwa na dereva wa
akiba.
Baada ya kubaini makosa hayo Waziri Mwakyembe aliwataka
madereva ambao walionekana kuwa na makosa kulipa faini ya papo hapo kwa
Sumatra, vinginevyo aliwataka Sumatra kuwafikisha mahakamani hata hivyo
madereva hao walikubali kulipa faini hiyo waliwasiliana na wamiliki wa
mabasi wanayofanyia kazi.
Akizungumza na maofisa wa Sumatra pamoja na
madereva, Dk Mwakyemba alisema makosa kama hayo yanaweza kusababisha
ajali za barabara na hivyo kupoteza maisha ya watu, kusababisha ulemavu
wa kudumu kwa abiria.
Alisema pia ajali zinasababisha uharibifu
wa mali na kwamba ataendelea kufanya ziara za namna hiyo mara kwa mara
ili kubaini makosa mengine.
Aidha aliwataka Sumatra pamoja na
kikosi cha usalama barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani na
kutowaonea aibu madereva watakaonekana kuwa na makosa kwani kwa kufanya
hivyo kutapunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa ni tishio hapa
nchini.
Kwa upande wake, mkuu wa usalama barabarani mkoani hapa,
Leonard Gyindo alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kimejipanga
katika kudhibiti ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi kabla ya gari
halijaondoka katika kituo hicho.
Gyindo alimpongeza Waziri
Mwakyembe kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa jitihada zake katika kusimamia
sheria hasa za usalama barabarani na kuahidi kuwa kikosi cha usalama
barabarani kitampa ushirikiano na kutekeleza maagizo yote atakayotoa.
Kwa
upande wa wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada
ya ziara hiyo walimwomba Waziri huyo kufanya ziara nyingine kituoni
hapo hasa nyakati za usiku na kushuhudia hali ya giza lililopo katika
kituo hicho.