Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
HII ndiyo Bongo bwana! Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu
uliopita, Simba, mpaka leo hawajapewa fedha zao za kutwaa taji hilo
ambazo ni shilingi milioni 42. Kinacholeta utata zaidi ni kitendo cha
wadhamini ambao ni kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, kudai
wameshawasilisha fedha hizo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo
nalo linadai halijapokea fedha kutoka kwa wadhamini. Simba kupitia kwa
ofisa habari wao, Ezekiel Kamwaga, walizungumza na gazeti hili juzi na
kulalamika kwamba kitendo kinachofanywa na TFF na wadhamini wa ligi kuu
kuwacheleweshea fedha hizo si sahihi, kwa kuwa walitarajia kuzitumia
wakati wa usajili. Kamwaga alilalama: “Ligi ilikuwa imepangwa na walijua
wazi lini inaisha, hivyo ingekuwa rahisi kutoa fedha hizo mapema.
Nashangaa kuona hadi sasa bado hatujapewa fedha hizo ili ziweze
kutusaidia katika maandalizi ya michuano ya Kagame.” TFF kupitia kwa
ofisa habari wao, Boniface Wambura, walisema wao wanasubiri wadhamini wa
Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Vodacom wapange siku maalum ya kutoa zawadi
za washindi. Championi lilipodadisi kwa mmoja wa viongozi wa juu wa
kampuni hiyo alisema: “Tumeshapanga hafla ambayo itafanyika Juni 30,
mahali patakapotangazwa baadaye, lakini fedha zote tayari
tulishazikabidhi kwa TFF siku nyingi na hatudaiwi.” Mbali na fedha hizo
za Simba, Azam nao hawajapewa fedha zao za ushindi wa pili ambazo ni Sh
milioni 17 na Yanga hawajapata milioni 11 kutokana na kuwa washindi wa
tatu.
SOURCE: GOLOBAL PUBLISHER