Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
MWENYEKITI wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka wananchi
kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao hata kama ni ya kutaka kuvunja
Muungano katika mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya. Kauli hiyo ya
Jaji Warioba imekuja kipindi ambacho kuna vuguvugu la kutaka Zanzibar
ijitenge, linalofanywa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam
(JUMIK), na kusababisha machafuko visiwano humo.
Jana, Jaji
Warioba akizungumza na waandishi wa habari kutangaza kuanza rasmi kazi
kwa tume hiyo tangu ilipozinduliwa rasmi April 13, mwaka huu, aliweka
wazi msimamo huo unaoondoa mkanganyiko katika suala hilo. Kumekuwapo
sintofahamu kuhusu msimamo wa Serikali juu ya Muungano, hasa baada ya
Rais Jakaya Kikwete kueleza suala hilo kama moja ya tunu za Taifa,
ambayo haitakiwi kujadiliwa kwa lengo la kuuvunja. Jaji Warioba
alifafanua kwamba, tume hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na
kwamba itakusanya maoni yote na kuyaratibu, ili kupata Katiba
wanayoitaka wananchi wenyewe. “Tume inafanya kazi kwa kufuata
sheria. Na kwa kuwa klatika mchakato ni lazima tuanze na Katiba ya
sasa, kwanza wananchi waseme upungufu wake. Wananchi wako huru
kupendekeza, kwa mfano, kuwepo kwa Serikali yaani Bunge na Mahakama,
labda wanataka tuwe na Rais dikteta, waseme,” alisema Jaji Warioba na
kuongeza: “Kuhusu Muungano, tutayapokea maoni yote. Kama wanataka mambo
ya Muungano yapunguzwe, au yaongezwe, Serikali moja au mbili au
wanataka tuvunje Muungano, yote tutayapokea. Tusiseme watu wamezuiwa,
hakuna aliyezuiwa.”
Akifafanua kifungu cha tisa cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayotumika katika mchakato huo, Jaji
Warioba alisema Katiba haiwezi kuundwa kama hakuna nchi, ndiyo maana,
suala la Muungano limewekwa kuwa la msingi. Kifungu hicho
kinazungumzia mambo ya msingi (tunu za taifa), ambayo Tume ya Katiba
itayazingatia wakati wa kukusanya maoni ya wananchi. “Muswada wa
kwanza uliyataja hayo mambo ya msingi kama matakatifu, lakini
marekebisho yaliyofuatia yalibadilisha na kuweka kuwa mambo ya msingi.
Tume inayazingatia kwa sababu huwezi kuunda Katiba kama hakuna nchi.
Katiba
tuliyonayo inasema Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,”
alifafanua Jaji Warioba. Kuhusu tume hiyo kufanya kazi Zanzibar kabla
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi,
Jaji Warioba alisema Katiba ya Zanzibar haisemi hivyo, badala yake
inaelekeza kutoa taarifa tu. “Utaratibu uliopo ni sheria kuwekwa
mezani, ndivyo ilivyo. Sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano zinatakiwa ziwekwe mezani, Baraza haliendi kujadili bali
linapewa tu taarifa,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:, “Sheria hii
ilitungwa Novemba mwaka jana na Baraza limekutana Januari mwaka huu.
Kwa
utaratibu wa kawaida ilitakiwa iwekwe mezani kwenye Baraza mwezi huo,
lakini kukawa na marekebisho mwezi Februari, baada ya hapo tukaipeleka.
Sisi tume wala hatuna wasiwasi kwa sababu hilo limeshapita.” Kifungu
cha 132 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinasema:
“Hakuna
sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika
Zanzibar mpaka Sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya muungano tu na
ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano. Na kifungu cha 132 (2) kinasema, “ Sheria kama
hiyo lazima ipelekwe mbele ya baraza la Wawakilishi na Waziri
anayehusika.”
Uratibu wa maoni
Kuhusu uratibu wa maoni ya
Katiba, Jaji Warioba alitaja maeneo manne muhimu yaliyopewa uzito
katika ukusanyaji wa maoni kuwa ni misingi ya Taifa ambayo ni uhuru,
haki, udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini
yoyote, ingawa wananchi wake wana uhuru wa kuabudu, huku eneo la pili
likiwa ni mamlaka ya wananchi.
“Kuna watu wanasema mamlaka ya
wananchi hayakufafanuliwa kama vile Serikali, Bunge na Mahakama, tume
ingependa kusikia maoni ya wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi,
wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee, vijana na
walemavu,” alisema. Aliyataja maeneo mengine kuwa ni malengo muhimu
na msingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali, kama inavyoelezwa katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya tisa na eneo la Haki za Binadamu
na wajibu wa jamii, kama inavyoelezwa katika sehemu ya tatu ya Katiba.
Marupurupu ya Tume/ Utaratibu
Akizungumzia
madai kwamba wajumbe wa tume hiyo wanalipwa marupurupu mengi, Jaji
Warioba japo hakufafanua mishahara ya wajumbe alisema hizo ni tetesi
zisizo na ukweli.
“Nimesikia ‘speculations’ (tetesi) nyingi
kuhusu hayo. Lakini, ninyi mtubane kwa kazi tuliyopewa ya kukusanya
maoni….Hapa kuna wengine wana mapato ya chini kuliko huko walikokuwa,
kwa kuwa tu wanaona umuhimu wa kulitumikia taifa lao… Sijui kila mtu
analipwa kiasi gani…,” alisema Jaji Warioba. Akizungumzia utaratibu wa
kazi wa tume hiyo, Jaji Warioba alisema kuwa tume hiyo itaanza kazi
katika mikoa minane ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja,
Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Aliongeza kuwa tume hiyo
itakuwa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya Katiba kwa
wananchi, ikiwa ni pamoja nakala 500,000 za Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar na nakala 500,000 za
Sheria ya Katiba ya mwaka 2012. Alisema baada ya kukusanya maoni hayo,
Tume itakutana na mabaraza ya Katiba na mwishowe rasimu ya Katiba
itafikishwa kwenye Bunge Maalum. Aliwataka waandishi wa habari
kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kushiriki katika mchakato
huo.
Vurugu za JUMIK
Hivi karibuni visiwa vya Zanzibar na
viunga vyake vilikumbwa na vurugu kubwa baada ya kundi la Uamsho
kufanya vurugu na kutaka visiwa hivyo vijitenge kuwa dola huru. Hata
hivyo, vurugu hizo zilidhibitiwa na Jeshi la Polisi, lakini juzi
zililipuka upya na polisi kulazima tena kutumia nguvu kuzidhibiti.
June 20, 2012
WARIOBA: RUKSA KUJADILI MUUNGANO, HATA WALE WANAOTAKA UVUNJWE WALETE MAONI YAO
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget