Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka
imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika Kusini na
sasa figo zake zimeanza kufanya kazi.Dk Ulimboka alipelekwa nchini huko
mwishoni mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kiasi cha
kusababisha figo zake kushindwa kufanya kazi.Katibu wa Chama cha
Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam
jana kwamba, hali ya Dk Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania
wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini
zinasema kwamba, hali ya Dk Ulimboka imezidi kuimarika tofauti na
alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa kwa polepole na
amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:
“Pia ameanza kuzungumza, anawatambua watu vizuri na zaidi amewaomba Watanzania wamuombee apone haraka.”
Awali,
chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba hali ya Dk Ulimboka
imeimarika kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa
kufanyiwa pamoja na vipimo vingine, kile cha usafishaji damu na figo
(Dalysis), mara kwa mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dk Ulimboka
alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.
Madaktari walisema kuwa,
kipimo hicho kililenga kupunguza kiwango cha sumu iliyoonekana kwenye
damu, ambayo haikutambulika mara moja kama ilitengenezwa ndani ya mwili
au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha kubaini tatizo hilo nchini.
Migomo hospitalini
Licha
ya huduma kurejea taratibu katika baadhi ya hospitali nchini, mgomo wa
madaktari bingwa umeendelea chini kwa chini.Pia jana, Serikali imewataka
madaktari wote walio katika mafunzo ya vitendo kuripoti Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, ifikapo Ijumaa.
Jana, wizara hiyo ilitoa
taarifa ikitaka madaktari wote nchini wanaofanya mafunzo kwa vitendo
(interns) ambao walipewa barua za kurudishwa wizarani, kuripoti Dar es
Salaam Julai 6, mwaka huu.
Mgomo wa madaktari bingwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umekuwa na utata baada ya kuwapo
taarifa mbili zinazokinzana.
Uongozi wa (MNH) kupitia kwa Msemaji
wake, Aminiel Aliegaeshi umetoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya
habari jana ukisema huduma za matibabu zinaendelea kama kawaida, lakini
kwa kiwango cha kati.
“Huduma hapa hospitalini zinaendelea
kutolewa kwa kiwango cha kati, wagonjwa ni wachache wanaokuja kutibiwa.
Madaktari Bingwa wote wameingia na kufanya kazi na Interns kumi na moja
wamefanya kazi,” alisema.
Jana waandishi wetu walishuhudia
baadhi ya huduma zikiendelea kutolewa kama kawaida katika hospitali hiyo
zikiwemo x-ray katika Taasisi ya Mifupa (Moi) na hospitali hiyo kuu.
Awali, huduma hiyo na nyingine zilisimama baada ya tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Lakini,
wakati Aliegesha akitoa taarifa hiyo, madaktari bingwa wamesisitiza
kuwa wako kwenye mgomo huku msemaji wao, Dk Cathrine Mng’ong’o akitaka
waandishi wa habari kulinganisha maneno hayo ya uongozi na hali halisi
hospitalini hapo.
“Mimi siwezi kujibu swali hilo (kama wako
kwenye mgomo au wamerudi), sababu sipo katika eneo la hospitali leo,
niko nyumbani. Wewe angalia kwa macho yako uone kisha linganisha maneno
hayo na hali halisi,” alisema Dk Mng’ong’o.Alipoulizwa kuwa kama jana
alikuwa zamu alijibu kwa kifupi kuwa madaktari bingwa hawana zamu na
hufanya kazi saa 24.
Madaktari hao juzi walitangaza mgomo wakitaka Serikali kuwarudisha kazini madaktari wote waliofukuzwa.
Uongozi
wa MNH ulisema, idara ambazo madaktari walikuwapo ni ya huduma za
dharura na katika vitengo vingine ilidaiwa kuwa walifika kwa kiwango
kikubwa.
Katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, hali
imezidi kuwa tete baada ya wagonjwa kuhamishiwa hospitali za binafsi
kutokana na kuzorota kwa huduma.Mkazi wa Sakina aliyejitambulisha kwa
jina moja la Manka, ambaye mtoto wake alikuwa amelazwa hospitalini hapo
akisubiri upasuaji alisema, amelazimika kumhamisha mtoto wake kutokana
na kukosa huduma.
Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo,
Eliringia Mlay alikanusha madai ya kuwapo kwa mgomo hospitalini hapo na
kusema kuwa, ulikuwapo awali lakini kwa sasa umekwisha na madaktari
wanaendelea na kazi kama kawaida. Hospitali binafsi
Hospitali ya
TMJ imeanza kutoa huduma ya tiba kwa baadhi ya wagonjwa waliokuwa
Muhimbili baada ya kuingia mkataba na Serikali ili kutoa huduma ya
matibabu katika kipindi ambacho madaktari wa Serikali wapo katika mgomo.
Msemaji
wa Hospitali hiyo, Huzaifa Seif alisema jana kuwa wagonjwa wanaotibiwa
katika hospitali hiyo ni wale wenye kadi za Bima ya Afya na wagonjwa
walioandikiwa rufaa kutoka MNH.
Hata hivyo, mmoja wa wagonjwa, Anaeli
Mbasha alisema ingawa Serikali imeingia mkataba na hospitali hiyo,
wagonjwa wengine wenye kipato kidogo wanashindwa kuhimili malipo.
Hospitali
ya Regency imekuwa na ongezeko la wagonjwa ikiaminika kuwa ni kutokana
na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa madaktari hospitalini hapo, Dk
Emmanuel Jonathan alisema wagonjwa ni wengi hasa kutoka Muhimbili.
Katika
Hospitali ya Aga Khan, baada ya wiki iliyopita kuwa na ongezeko la
wagonjwa kwa asilimia 15, idadi hiyo imepungua kati ya jana na
juzi.Mkurugenzi wa Tiba wa Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema:
“Ongezeko kubwa lilikuwa katika vipimo ambavyo vinapatikana katika
Hospitali ya Muhimbili na hapa (Aga Khan), peke yake kwa mfano MRI
(Magnetic Resonance Imaging).”
Geofrey Nyang'oro, Victoria
Mhagama, Halima Shebuge, Zakhia Abdallah, Sam Jacob (SJMC), Pamela
Chilongola na Sam Jacob, Moses Mashalla, Arusha.
Source: mwananchi
July 4, 2012
Figo za Dk Ulimboka zaanza kufanya kazi
Millionfortune.com
MCHANGANYIKO
Facebook Blogger Plugin by JustNaira.com | Get Widget