Tweeted this
Like this, be the first of your Friends
Ofisa Uchumi wa Mkoa wa Tanga na Mweka Hazina wa Chuo cha VETA cha
Jijini hapa pamoja na Maofisa wengine wanne Waandamizi wa Wilaya ya
Kilindi , wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani 05 Julai 2012 kujibu tuhuma
mbalimbali za ubadhirifu zinazowakabili.
Akizungumza na Gazeti
hili jana mmoja wa Maofisa Waandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga, ambaye
aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema watumishi hao wanatuhumiwa kwa
makosa mbalimbali.
Katika kesi hiyo Namba: ECC. 05/2012, Ofisa
huyo alitaja makosa hayo kuwa ni matumizi mabaya ya nyaraka za Serikali,
kumdanganya mwajiri wao, uhujumu uchumi, kughushi nyaraka na
kuisababishia serikali hasara.
Aliwataja maofisa hao kuwa ni
pamoja na Annunsiata Anselm Lyimo ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ambaye sasa ni Mchumi katika Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Benedict Philip Mburi, Mhasibu wa Veta Tanga.
Wengine
ni Rowland Michael Lema, Ofisa Misitu wa Halmashauri ya wilaya ya
kilindi, Bakari Ali Mnaguzi, Ofisa Misitu Msaidizi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilindi, Waziri Ali, Mhasibu wa Mradi wa PFM Halmashauri ya
Wilaya ya Kilindi na Eniyoye Chezue Mrinji, Afisa Misitu Hifadhi Wilaya
ya kilindi.
"Tarehe 21/06/2012 kesi ilifunguliwa mahakamani
ambapo washitakiwa wanne tu walifika mahakamani . TAKUKURU Wilaya ya
Klindi inafanya jitihada ya kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Handeni tarehe 05/07/2012, kwa vile hapa
Kilindi hatuna Mahakama ya Wilaya tunategemea ile ya Handeni," alisema
Ofisa huyo.
Alisema sababu za tuhuma hizo ni uendeshaji mbaya wa
makosa yaliyotajwa wakati wa kutekeleza Mradi wa usomamizi Shirikishi
wa Misitu (PFM) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mwaka 2006.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Tanga ili kuzungumzia suala hilo, hazikuweza kufanikiwa kwa kuwa hakupatikana.
Tukio
hilo la viongozi hao kukamatwa limekuja siku chache baada ya Ofisa wa
Misitu hifadhi wilayani Handeni, Rashidi Kiure, kufikishwa katika
Mahakama hiyo ya Wilaya ya Handeni na Takukuru wilayani humo, kwa tuhuma
za ubadhirifu wa mali ya umma.