Wauguzi
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakimpeleka Mgonjwa wodi ya Sewahaji
jana baada ya kushindw akufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Mifupa
(MOI) jana kutokana na mgomo wa madaktari. Picha na Juliana Malondo
Waandishi Wetu
WAKATI
uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ukitangazia umma kwamba
huduma katika taasisi hiyo zimerejea kama kawaida, uchunguzi wa kina wa
Mwananchi umebaini kwamba huduma katika taasisi hiyo na Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), bado zinasuasua.Juzi, uongozi wa MOI ulitoa
taarifa kwa umma ukisema mgomo wa madaktari bingwa uliokuwa umetangazwa
awali ulikwisha, huku uongozi wa MNH nao ukisema huduma zimerejea katika
kiwango cha kati na kutaka wagonjwa waendelee na huduma kama kawaida.
Uchunguzi
uliofanywa jana katika taasisi hiyo ya MOI na MNH na taarifa kutoka
vyanzo mbalimbali, ulionyesha taarifa hizo mbili zinapingana na hali
halisi ya utoaji huduma na mahudhurio ya wagonjwa katika hospitali hizo
mbili.
Uchunguzi
huo ulibaini kwamba, kitendo cha uongozi wa MOI kuwatembeza waandishi
wa habari kujionea huduma za upasuaji juzi, kilikuwa ni mchezo wa
kupanga ili kuonyesha umma kuwa huduma zimerejea.
Chanzo
chetu cha habari kilisema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence
Museru alifanya jukumu la kuwapigia simu madaktari ambao anawajua ili
kumnusuru na adha hiyo ya mgomo wa madaktari.
“Mkurugenzi
(Profesa Museru), aliwapigia simu madaktari akiwataka kufika kufanya
upasuaji ili nyie waandishi mkipiga picha mwonyeshe kuwa huduma
zimerejea,” kilisema.
Hata
hivyo, alipoulizwa Profesa Maseru alijibu: "Hatuna sababu ya kudanganya
mtu. Lakini, kama unataka maelezo zaidi naomba uje ofisini."
Juzi
akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya MOI, Profesa
Charles Mutalemwa alisema toka Jumatatu wiki hii madaktari 79 wamerejea
kazini.
Profesa
Mutalemwa alisema madaktari bingwa waliorejea ni 18 na 61 ni madaktari
wa kawaida na walioko mafunzoni hivyo huduma zinaendelea kuimarika kadri
siku zinavyoendelea.
Mwananchi
lilifika katika kitengo hicho kujionea hali halisi ya huduma na kukuta
wagonjwa wakipangiwa kufika hapo mwanzoni mwa mwezi ujao.
Kauli za wagonjwa
Aidan
Kisanga ambaye alifika katika kliniki kutokana na tatizo la kuvunjika
mguu, alisema, licha ya kutakiwa kuonana na dakatri jana, imeshindikana.
“Nimeambiwa
nirejee hapa Juni 30 mwaka huu au kama nitasikia taarifa katika vyombo
vya habari kuwa huduma imerejea. Inaniuma kwani mguu wangu unaniuma na
sijui nitafanya nini,” alisema Kisanga.
Jakobo
Chacha mkazi wa Kitunda, alisema alifika hospitalini hapo saa 11.30
asubuhi jana na kupewa namba 26, lakini hakupata matibabu baada ya
mhudumu ambaye hakumfahamu, kuwatangazia kuwa hakuna huduma kutokana na
ukosefu wa madaktari.
“Tulitangaziwa
kuwa tuondoke na waliokwishalipia huduma wabaki. Wasiolipia tulikuwa
tunapangiwa kila mtu na tarehe yake,” alisema Chacha na kuongeza:
"Jana
(juzi), tumeambiwa madaktari wamerejea na kutakiwa kufika kupata huduma
kumbe ilikuwa ni uongo, wanatuambia twende hospitali binafsi sasa kama
sisi wa hali ya chini si tutakufa?" alihoji.
Ezekiel
Mkandainda ambaye amelazwa katika wodi ya Sewahaji, MNH, alisema mgomo
bado unaendelea na jambo hilo limefanya baadhi ya wagonjwa kufariki na
wengine kuamua kuondoka kutokana na kukosekana madaktari.
“Mwandishi,
madaktari bado wanaendelea na mgomo, leo (jana) ilikuwa siku yangu ya
kuonana na daktari, lakini hatujamwona daktari yeyote aliyepita wodini
kwetu zaidi ya wauguzi,” alisema na kuongeza:
“Wagonjwa
wengi wameondolewa na ndugu zao kwenda kutibiwa kwenye hospitali za
watu binafsi. Mimi nimetoka Mkoa wa Kigoma nina matatizo ya kibofu cha
mkojo natakiwa nifanyiwe upasuaji, lakini hadi leo sijafanyiwa.”
Mgonjwa
mwingine aliyelazwa katika wodi ya Mwaisela, MNH, Aisha Abdallah
alisema wagonjwa waliopo katika wodi hiyo ni wachache kutokana na
wengine kuondolewa na ndugu zao baada ya kukosekana madaktari.
Uongozi MNH
Ofisa
Habari wa Hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alisema kusuasua kwa
huduma hizo kumetokana na madaktari hao kuanza kazi Julai 2 mwaka huu
ambao ni wachache.
“Kuhusu
huduma kusuasua ndiyo kwanza madaktari wameanza kazi wiki hii siku ya
Jumatatu hivyo, tusitegemee huduma kuwa nzuri kama mwanzo. Madaktari
watakapokuwa wengi huduma zitatolewa kama kawaida,” alisema Aligaesha.
KCMC, Mount Meru bado
Wakati
huo huo, madaktari zaidi ya 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC waliondoka jana kwenda jijini Dar es
Salaam na kusababisha huduma hospitalini hapo kuzorota.
Mwandishi
wa habari hizi aliyetembelea hospitali hiyo jana, alishuhudia idadi
ndogo ya wagonjwa walioko wodini huku kliniki zote zikiwa zimesitisha
utoaji huduma kutokana na mgomo huo.
Daktari
mmoja bingwa aliyekutwa akitoa huduma, aliliambia gazeti hili kuwa, kwa
sasa hawapokei wagonjwa wa rufaa wala kuendesha upasuaji wa kawaida
isipokuwa upasuaji wa dharura tu.
“Uamuzi
wa kuwarudisha resident doctors (wanaosomea ubingwa) kwa mkuu wa chuo
haukuwa wa busara…,wewe unaona interns doctors hawapo halafu unawaondoa
tena na resident,”alilalamika.
Madaktari
wanaosomea ubingwa wako kati ya 50 na 60 hivyo ukichanganya na
madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo, hospitali hiyo
inakabiliwa na upungufu wa madaktari karibu 140.
Taarifa
zilidai kuwa, madaktari walioko katika mafunzo kwa vitendo wapatao 80
waliondoka mjini Moshi jana kwenda Dar es Salaam baada ya kutakiwa
kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya leo.
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa KCMC, Dk Moshi Ntabaye ameshikilia msimamo wa kutotoa
ushirikiano kwa wanahabari hata pale anapofuatwa ofisini au kupigiwa
simu yake ya kiganjani.
Mount Meru warejea kazini
Hospitali
ya Mkoa wa Arusha imesitisha zoezi la kuwaondoa madaktari 26 waliopo
katika mafunzo kwa vitendo katika hospitali hiyo baada ya wote kusitisha
mgomo baridi na kuendelea na kazi...
from www.mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment
Toa maoni yako hapa!