Mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam,Dk.Kitila Mkumbo (wa tatu mwenye miwani) akiingia kwenye viwanja vya mahakama ya hakimu mkazi mjni Singida kusomewa shitaka ya kutoa lugha ya matusi kwa mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi Mwigullu Nchemba.
Mhadhiri wa chuo kikuu Dar-es-salaam, Dk.Kitila Mkumbo (kushoto) akitetea jambo na wakili wake Raymond Kimu muda mfupi kabla hajasomewa shitaka lake la kutoa lugha ya matusi kwa mbunge wa jimbo la Iramba magharibi Mwigullu Nchemba.
 Na Nathaniel Limu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na mshauri wa Chama cha CHADEMA Dkt. Kitila Mkumbo (41), amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida, akituhumiwa kutoa lugha ya matusi kwa mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi (CCM)Mh.  Mwigullu Lameck Nchemba.
Dkt. Mkumbo ameunganishwa katika kesi hiyo na Afisa Sera na Utafiti wa CHADEMA makao makuu Mwita Waitara Mwikwabe (37) ambaye alisomewa shitaka hilo Julai 16 mwaka huu.
Mapema mwanasheria wa serikali Maria Mudulugu, alidai mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ruth Massamu kuwa mnamo Julai 14 mwaka huu, mshitakiwa Dkt. Mkumbo alitoa lugha ya matusi kwa mbunge wa jimbo la Iramba magharibi kuwa ni malaya, mzinzi na ni ‘the comedy’ huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Mwanasheria Mudulugu amesema kuwa mshitakiwa alitoa lugha hiyo ya matusi kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika kwenye viwanja vya kituo cha mabasi cha kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Mshitakiwa amekana shitaka hilo na yupo nje baada ya kudhaminiwa na watu wawili na kesi hiyo itatajwa tena Julai 30 mwaka huu.
Mshitakiwa Dkt. Kitila Mkumbo anatetewa na wakili wa kujitegemea mjini Singida Raymond Kimu.
Wakati huo huo, vijana wawili wakazi wa kata ya Ndago Paulo Nashakigwa Shumu (27) na Emmanuel John Shilla (24), wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida wakituhumiwa kushiriki kumuuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (VCCM) Yohana Mpinga (30).
Mudulugu alidai mbale ya hakimu Massamu kuwa mnamo Julai 14 mwaka huu katika kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago, washitakiwa wote kwa pamoja wakitumia fimbo na mawe, walimpiga Yohana na kusababisha kifo chake.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Washitakiwa hao wameunganishwa na wenzao 12 ambao wamesomewa shitaka hilo la mauaji  Julai 16 mwaka huu.
Kesi hiyo itatajwa tena julai 30 mwaka huu.